| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
'Wamepata vidonda mwilini' — wanaharakati wasimulia mateso waliyopitia walipotekwa na Israel
Wanaharakati wanatoa ushahidi wa mateso waliyopitia wakiwa chini ya ulinzi wa Israel, huku baadhi wakisimulia madhila waliyopitia kuwa ni mabaya kuliko hata ya wanayofanyiwa wanyama.
'Wamepata vidonda mwilini' — wanaharakati wasimulia mateso waliyopitia walipotekwa na Israel
Wanaharakati kutoka Msafara wa Meli wa Global Sumud wakifarijiana baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Istanbul. / AP

Wanaharakati wa msafara wa meli wa Global Sumud Flotilla, ambao walitekwa na Israel walipokuwa katika maji ya kimataifa wakielekea Gaza, wamesema ukiukaji na unyanyasaji waliofanyiwa katika mikono ya wanajeshi wa Israel hauwezi kulinganishwa na wanayopitia Wapalestina.

Wanaharakati hao, ambao waliletwa mjini Istanbul Alhamisi kwa ndege tatu za Shirika la Ndege la Uturuki baada ya kuvamiwa na kushikiliwa na Israel wakiwa katika maji ya kimataifa, wamezungumza na Shirika la Anadolu kuhusu waliyopitia.

Mwanaharakati kutoka Canada Ehab Lotayef ameonesha mkono wake uliofungwa bandeji huku akisimulia walivyovamiwa na Israel wakiwa katika boti.

"Mwanajeshi mmoja hakupenda kuona nikiwasaidia watu kwa kuwapa maji. Kwa hiyo, alikuja na kunidunga mkononi mwangu," amesema Lotayef.

Amesema kuwa alipoteza hisia katika mkono wake uliojeruhiwa na kuongeza kuwa wanaharakati walikabiliwa na unyanyasaji mkubwa, huku baadhi wakivunjika mbavu.

"Tulipigwa sana, sana, ilikuwa mbaya. Haikuwa kwa lengo la kujikinga. Ilikuwa ni kipigo cha kutuadhibu. Walikuwa wanatuadhibu," amesema.

Wakati wakiwa chini ya ulinzi wa Israel, Waziri Itamar Ben-Gvir aliweka video katika mitandao ya kijamii inayomuonesha akiwakejeli wanaharakati hao, waliopigishwa magoti huku mikono yao ikiwa imefungwa.

Video imeibua hasira

Katika bara lote la Ulaya, serikali zimewataka mabalozi wa Israel kulaani video hiyo. Italia imetaka kuombwa msamaha, Hispania imesema kuwa katu haitavumilia kudhalilishwa kwa raia wake, na Ufaransa imetaka kuachiwa huru kwa wanaharakati wote wanaoshikiliwa.

Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, amesema Ben-Gvir "amesaliti" utu wa taifa lake.

"Waangalie sasa. Angalia wanavyoonekana, sio mashujaa wala chochote," alisema Ben-Gvir katika video huku akipita kwa wanaharakati akiwa amebeba bendera kubwa ya Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, anayeongoza serikali yenye kiwango kikubwa cha unyanyasaji katika historia, amesema tabia ya Ben-Gvir haiwakilishi "misingi ya Israel".

Lakini Ben Gvir ameonekana kujitetea, na kuziita picha hizo, "fahari kubwa."

'Wanyama wana afadhali'

Bilal Kitay, raia wa Uturuki, amemkumbatia mke wake.

Hii ni mara yake ya pili kuwa katika msafara wa "Flotilla" kuelekea Gaza, amekuwa katika boti na wanaharakati wengine 10.

Wamesisitiza kwamba, uvamizi wa Israel wakiwa katika maboti ulikuwa "mbaya zaidi kuliko wa awali" wa Aprili.

"Walitushambulia," amesema.

"Kila mmoja wetu alipigwa, wanawake na wanaume, ndicho wanachopitia Wapalestina kila wakati," amesema, imeripoti AFP.

"Kwa bahati mbaya, hata wanyama wanawachukulia vizuri. Wao pekee yake wanajichukulia kuwa ndio binadamu," amesema.

Kitay anapanga kurudi tena katika msafara mwengine.