Kliniki za Sudan zinakabiliwa na upungufu wa dawa kutokana na vita vya Israel dhidi ya Iran

Vita vinavyozidi kuongezeka kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimetikisa misururu ya ugavi duniani, na kufungwa kwa anga na kusitishwa kwa usafirishaji wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

By
Sudan inatishiwa upungufu wa dawa / Reuters

Vifaa vya matibabu kwa kliniki zinazokabiliana na mzozo wa kibinadamu nchini Sudan vinaweza kuisha ndani ya wiki mbili iwapo usafirishaji hautarekebishwa kwa haraka baada ya kukatika kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, shirika la kutoa misaada la Save the Children lilisema.

Vita vinavyozidi kuongezeka kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimetikisa misururu ya ugavi duniani, na kufungwa kwa anga na kusitishwa kwa usafirishaji wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

Takriban kliniki 90 zinazosimamiwa na serikali ya Sudan zinazohudumia takriban wagonjwa 400,000 zinategemea usambazaji wa dawa, chanjo na lishe kutoka kwa shirika la misaada, bila njia mbadala ya ndani ya nchi, mkurugenzi wa kimataifa wa shirika la Save the Children wa usalama wa ugavi, Willem Zuidema, aliiambia Reuters.

Mgogoro wa miaka mitatu wa Sudan umewakosesha makazi mamilioni ya watu na kusababisha moja ya machafuko makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

"Tuna wiki kadhaa za kufanya upangaji mpya huu kabla ya akiba kuisha. Muda unayoyoma," Zuidema alisema, akiongeza kuwa mara tu akiba inapoisha wagonjwa hawataweza kupata usaidizi wa kimsingi wa afya.

Dawa hizo, ambazo ni pamoja na viuavijasumu, dawa za malaria, dawa za maumivu na homa, na dawa za sindano za watoto, kwa kawaida huingia kupitia Bandari ya Sudan na kusafiri kwa barabara hadi maeneo ya Darfur.

Mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa Tom Fletcher alisema wiki iliyopita mzozo wa Mashariki ya Kati unahujunmu njia za ugavi wa kibinadamu, huku Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Gaza zikiwa chini ya shinikizo kubwa zaidi.