Utajiri wa mabilionea wa Kiafrika unakua kwakasi. Imeongezeka kwa angalau 56% katika kipindi cha miaka mitano pekee.
Tofauti na hilo, maskini wanazidi kuwa maskini pia. Kulingana na ripoti ya 2025 ya Oxfam International, watu wanne tajiri zaidi barani Afrika walikuwa na utajiri zaidi ya watu milioni 750 kwa pamoja. Hiyo ni nusu ya wakazi wote wa bara.
Afrika haikuwa na bilionea aliyeorodheshwa hadharani kufikia 2000. Sasa kuna angalau 23.
Kulingana na Forbes, thamani yao kwa jumla ni $126.7 bilioni kufikia Mei 2026. Hiyo ni asilimia 21 kutoka mwaka uliopita.
Kutoka kwa Aliko Dangote wa Nigeria na Abdul Samad Rabiu hadi Johann Rupert na Nicky Oppenheimer wa Afrika Kusini, na Nassef Sawiris wa Misri na wengineo, matajiri wakubwa wanaendelea kujenga himaya za biashara.
Ukweli wa ulimwengu
Lakini hili si suala la Kiafrika tu. Ni ukweli wa kimataifa. Ripoti ya Kukosekana kwa Usawa Duniani ya 2026 na Maabara ya Kukosekana kwa Usawa Duniani inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inasema tofauti ya utajiri inasalia kuwa "iliyokithiri na inaendelea" ulimwenguni kote.
Inasema "asilimia 10 ya juu ya watu wanaopata mapato ulimwenguni huchukua zaidi ya 90% iliyobaki."
Lakini kwa nini?
Ripoti ya Kukosekana kwa Usawa Duniani inasema tatizo hilo linatokana na kutozwa ushuru hafifu kwa matajiri, mkusanyiko mkubwa wa mtaji, na ukosefu wa usawa wa elimu na fursa.
Baadhi ya matajiri wakubwa pia hutumia "ushawishi wa kisiasa" kushawishi serikali. Hii inawaruhusu matajiri kuzuia mageuzi ambayo yanaweza kuwanufaisha maskini, ili kulinda maslahi yao ya biashara.
Biashara zao pia huchangia uzalishaji mwingi wa kaboni ambao huchafua mazingira na kuwakumba maskini zaidi.
Zaidi ya watu milioni 460 barani Afrika walikuwa wakiishi katika ‘’umaskini uliokithiri’’ mwaka wa 2025. Hiyo ni kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Mifumo ya kifedha
Wataalamu wanasema umaskini si ukosefu wa pesa katika jamii. Kuna pesa nyingi. Changamoto ni jinsi inavyotiririka. Baadhi ya matajiri hutengeneza ajira, kutoa michango, na kufadhili elimu na huduma za afya.
Lakini watafiti wanasema mifumo ya fedha ya kimataifa ni mbovu, ikiruhusu matajiri wakubwa kujilimbikizia mali kwa urahisi zaidi. Usawa huo unahitaji kurekebishwa. Ripoti ya Kukosekana kwa Usawa Duniani inasisitiza kuwa hii sio tu kuhusu takrima.
Lazima kuwe na upatikanaji wa elimu kwa wote - hakuna tofauti kati ya watoto wa matajiri na maskini.
Pia inatetea kukomesha mifumo ya kodi ambayo inapendelea matajiri, na uwekezaji mkubwa wa ndani ili kuunda nafasi nyingi za kazi, wakati serikali zinatekeleza sera rafiki za kiuchumi na kukabiliana na rushwa.


















