Jakaya Kikwete ateuliwa kuwa Mwakilishi Maalumu wa Pembe ya Afrika, Bahari ya Shamu

Mwenyekiti wa Tume ya Afrika, ameonesha matumaini na imani yake kubwa kwa Kikwete, akigusia uzoefu, uongozi na busara zake, akisisitiza kuwa, atakuwa na mchango mkubwa kutatua changamoto zenye kuzikabili maeneo hayo mawili.

By
Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete./Picha:@jmkikwete

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf amemteua Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kama Mwakilishi Mkuu wa eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

Uteuzi huo utamfanya kiongozi huyo wa zamani wa Tanzania, atatue changamoto sa kisiasa, amani na usalama katika maeneo hayo, huku jukumu akifanya kazi kwa karibu na Umoja wa IGAD, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Machi 25, 2026 na msemaji wa tume hiyo, uratibu wa pande hizo ni wa muhimu, kwa kuzingatia umuhimu wa kimkakati wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu katika nyanja ya biashara ya kimataifa na utulivu mzima wa bara la Afrika.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa Tume ya Afrika, alionesha matumaini na imani yake kubwa kwa Kikwete, akigusia uzoefu, uongozi na busara zake, akisisitiza kuwa, atakuwa na mchango mkubwa kutatua changamoto zenye kuzikabili maeneo hayo mawili.