| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mwanadiplomasia wa Ubelgiji apinga kushtakiwa kuhusiana na mauaji ya Patrice Lumumba wa Congo
Etienne Davignon alitakiwa mapema mwezi huu kufikishwa mahakamani kwa “kushiriki katika uhalifu wa kivita” kwa kosa la “kumfunga na kumhamisha" Patrice Lumumba kinyume cha sheria.
Mwanadiplomasia wa Ubelgiji apinga kushtakiwa kuhusiana na mauaji ya Patrice Lumumba wa Congo
Patrice Lumumba alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa DR Congo baada ya kupata uhuru wake mwaka 1960. / Wengine / Others
tokea masaa 17

Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Ubelgiji, Etienne Davignon mwenye umri wa miaka 93, amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumfikisha mahakamani kuhusiana na mauaji ya mwaka 1961 ya kiongozi wa uhuru wa Congo, Patrice Lumumba, wakili wake alisema siku ya Ijumaa.

Akiwa mwanadiplomasia chipukizi wakati huo, Etienne Davignon ndiye pekee aliye bado hai kati ya Wabelgiji 10 wanaotuhumiwa na familia ya kiongozi huyo wa Congo kwa kushiriki katika mauaji yake.

“Bwana Davignon ameamua kukata rufaa,” wakili Johan Verbist aliliambia shirika la AFP.

Davignon alitakiwa mapema mwezi huu kufikishwa mahakamani kwa “kushiriki katika uhalifu wa kivita” kutokana na kosa la “kumfunga na kumhamisha kinyume cha sheria” Patrice Lumumba, aliyekuwa akichukuliwa kama mfungwa wa vita wakati huo, na pia kunyimwa haki ya kusikilizwa mahakamani.

Davingon, aliyewahi pia kuwa kamishna wa Ulaya anashutumiwa kwa “matendo ya kudhalilisha na kushusha hadhi,” ingawa hashtakiwi kwa kuhusika moja kwa moja katika mauaji ya Lumumba.

Waziri mkuu wa kwanza wa Congo

Lumumba, mkosoaji mkali wa utawala wa ukoloni wa Ubelgiji, alikua waziri mkuu wa kwanza wa nchi yake baada ya kupata uhuru mwaka 1960.

Hata hivyo, aligombana na wakoloni wa zamani ya pamoja na Marekani, na akaondolewa madarakani kupitia mapinduzi miezi michache tu baada ya kuingia madarakani.

Aliuawa tarehe 17 Januari 1961 akiwa na umri wa miaka 35 tu, katika eneo la kusini la Katanga, kwa msaada wa mamluki wa kutoka Ubelgiji — na mwili wake kuyeyushwa kwa tindikali.

Iwapo kesi hiyo itaendelea, Davignon atakuwa afisa wa kwanza wa Ubelgiji kufikishwa mbele ya sheria katika kipindi cha miaka 65 tangu kifo cha Lumumba.

Kikao kipya cha faragha kitafanyika ambapo mawakili wa pande zote watapambana kisheria.

Iwapo uamuzi wa mahakama utathibitishwa, kesi ya Davignon inaweza kuanza mapema Januari 2027, kulingana na Christophe Marchand, wakili wa watoto wa Lumumba.

CHANZO:Reuters