Rais wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, anawasili nchini Tanzania leo kwa ziara rasmi ya siku nne inayolenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Namibia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Juni 20, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao watajadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa nchi hizo mbili.
Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya kikao hicho.
Akiwa nchini Tanzania, Rais Nandi-Ndaitwah pia atatembelea eneo la Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam pamoja na kambi ya wapigania Uhuru wa Harakati za Ukombozi Barani Afrika iliyopo Kongwa, mkoani Dodoma.
Ziara hiyo, ambayo ni ya kwanza kwa Rais Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania tangu aingie madarakani, inatarajiwa kuhitimishwa Juni 22, 2026.









