| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Afrika Mashariki yatakiwa kujiandaa na athari za El Nino
Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wataalamu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Maandalizi na Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Mvua Zinazotarajiwa za El Niño Kali
Afrika Mashariki yatakiwa kujiandaa na athari za El Nino
Wajumbe kutoka EAC waliokutana kujadili hatari ya El Nino kwa kanda, jijini Nairobi

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, zikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, uharibifu wa miundombinu na kuathirika kwa biashara na maisha ya kawaida ya wananchi.

Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wataalamu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Maandalizi na Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Mvua Zinazotarajiwa za El Niño Kali, unaofanyika Nairobi, Kenya, kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2026.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa wataalamu  umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala.

‘‘Utabiri unaonesha uwezekano wa mvua kunyesha kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2026, hali inayohitaji maandalizi ya haraka na hatua za pamoja,’’ alisema Julius Twinamatsiko, mratibu wa mradi wa pamoja wa sekta za Usalama wa Chakula na Lishe nchini Uganda;

Amezitaka nchi wanachama kubaini maeneo hatarishi katika miundombinu ya usafirishaji, kuandaa njia mbadala, kuhakikisha upatikanaji wa chakula na malisho ya mifugo, pamoja na kuimarisha huduma za afya na ufuatiliaji wa magonjwa yanayoweza kuenea kutokana na mafuriko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Sekretarieti ya EAC amesisitiza kuwa athari za El Niño zinaweza kuhatarisha amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi, hivyo juhudi za kila nchi zinapaswa kuunganishwa kupitia mpango wa pamoja wa kikanda.

Mkutano huo unalenga kutathmini uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na athari zinazotarajiwa, kubaini mapungufu na kuandaa mpango wa uratibu wa kikanda utakaosaidia kulinda maisha ya wananchi, huduma muhimu na shughuli za biashara katika Afrika Mashariki.

CHANZO:TRT Afrika Swahili