Kufikia sasa Uturuki imefikisha misaada katika nchi 85 kwenye mabara matano kupitia mpango wa misaada ya kimataifa inayoratibiwa na Idara ya Majanga na Dharura (AFAD) chini ya wizara ya mambo ya ndani.
AFAD inaendelea na shughuli za uokoaji na misaada siyo tu nchini Uturuki lakini pia katika kanda tofauti duniani ikiwa sehemu ya juhudi zake za diplomasia katika majanga.
Chini ya uratibu wa AFAD, Uturuki imetoa misaada kwa nchi na jamii ndani ya mabara matano ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, dawa na vifaa muhimu, pamoja na msaada wa fedha, usaidizi na vifaa vya uokoaji.
Kulingana na taarifa iliyoandaliwa na Anadolu, shughuli kubwa ya Uturuki kwa misaada ya kimataifa ilifanyika Gaza.
Idara ya AFAD inasema tani 109,332 za misaada zilipelekwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya Israel kwa kutumia ndege 14 na meli 21.
Ikiwa sehemu ya misaada, jumla ya milioni $7.5 zilitolewa, ikiwemo milioni $7 na AFAD na $500,000 kutoka kwa Shirika la Hilali Nyekundu la Uturuki.
Ikiwa sehemu ya juhudi za misaada kwa Afghanistan, tani 11,739 za misaada zilipelekwa kupitia safari 25 za Hisani za Treni.
Ndege sita za mizigo pia ziliandaliwa kwa ajili ya nchi hiyo.
Sudan ilipata tani 10,206 za misaada na mahema 30,000 yalipelekwa kwa meli sita.
Uturuki pia ilipeleka tani 9,079 za misaada nchini Pakistan, tani 3,000 nchini Somalia na tani 730 Lebanon.
Bangladesh ilipata vifurushi 64,992 vya misaada, huku Bosnia na Herzegovina ikipewa nyumba za kontena 60, pamoja na mafuta, vifaa vya msingi, majenereta na bidhaa zingine muhimu.
Kufikia sasa, malori 13,938 ya misaada yamepelekwa nchini Syria.
Zambia ilipokea vifaa vya misaada vyenye thamani ya $25,000 vifurushi 600 vya chakula, huku misaada ya thamani ya $54,070 ikifikishwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na $60,000 nchini Burundi.
Moja ya shughuli za hivi karibuni za misaada ya kimataifa za Uturuki zilifanyika kwa ajili ya Venezuela.
Kufuatia mitetemeko miwili ya viwango vya 7.2 na 7.5 mwezi Juni, misaada ilipelekwa eneo hilo kwa ndege mbili za kijeshi chini ya uratibu wa AFAD, kwa maagizo ya Rais Recep Tayyip Erdogan.
Shehena hiyo ilijumuisha mahema 275 yaliyotolewa na AFAD na tani saba za dawa zilizotolewa na wizara ya afya.
Jumla ya tani 30 za misaada zilipelekwa nchini Venezuela.
Kufuatia mafuriko nchini Hispania, Uturuki pia ilitoa kontena 250 kwa ajili ya taka za plastiki, kila moja ikiwa na uwezo wa lita 1,100, na magari mawili ya kufanya usafi barabarani.





















