Mgogoro unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran umeanza kuathiri masoko ya kimataifa pamoja na usafirishaji wa mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Mgogoro huo ulianza rasmi Februari 28, 2026 ambapo Iran imekuwa ikilipiza kwa kufanya mashambulizi.
Athari imeonekana zaidi baada ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz huku anga ikifungwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Misaada kwa Gaza na Sudan inasimama na gharama zinapanda kwa ajili ya msaada kwa mamilioni ya wanaokabiliwa na janga la njaa duniani kote.
"Watu wanaohitaji msaada sana watalazimika kusubiri kwa muda mrefu," alisema Jean-Martin Bauer, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula katika Mpango wa Chakula Duniani.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema hali hii imechangia ucheleweshaji wa kupeleka msaada huku gharama za uwasilishaji zikiongezeka wakati ambapo tayari ufadhili umepungua.
Tayari, mahema, maturubai na taa zinatakiwa kutumwa katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa na Israel ya Gaza na Ukingo wa Magharibi zimekwama, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM lilisema.
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu, IFRC na Hilali Nyekundu, RCS, haziwezi kuhamisha vifaa vya kusaidia Shirika la Hilali Nyekundu ya Irani kutoka kituo chake cha Dubai ambapo kuna akiba ya dharura yenye thamani ya dola milioni 13, alisema Cecile Terraz, Mkurugenzi katika IFRC.
Kundi hilo haliwezi kuhamisha vitu kupitia bandari ya Jebel Ali - kituo kikubwa zaidi cha makontena katika eneo hilo, ambacho kilishambuliwa.
Operesheni za kitovu cha Shirika la Afya Duniani Dubai pia zimesitishwa, Mkurugenzi wa eneo hilo Hanan Balky alisema, na kuzuia maombi 50 ya dharura kutoka kwa nchi 25 hivyo kutatiza shughuli kama vile chanjo ya polio.
Wafanyabiashara wakubwa duniani wametangaza malipo ya dharura ya takriban $3,000 kwa kila kontena, limesema Shirika la IOM.
Mashirika ya IOM, UNHCR, IFRC, WFP, WHO na UNICEF, ambayo yanatumia maghala katika Kituo cha Kibinadamu cha Dubai yanakabiliwa na changamoto ya kuhamisha vitu na kuvipeleka sehemu zinazohitajika.










