Afrika Kusini yabaini zaidi ya wafanyakazi hewa 4,000 miongoni mwa wafanyakazi wa serikali
Mamlaka zinasema malipo ya ulaghai yamefanyika kwa wafanyakazi hewa, kwa kutumia namba za vitambulisho vinazofanana, na hata watu waliofariki.
Afrika Kusini imebaini zaidi ya wafanyakazi hewa 4,000 katika malipo ya mishahara ya serikali kama sehemu ya ukaguzi wenye lengo la kupunguza ufisadi na kupunguza mzigo wa malipo ya umma.
Hazina ya Taifa imesema tathmini ya mfumo wa Mishahara Serikalini (PERSAL) imeonesha kesi 4,323 zinazoshukiwa, huku uhakiki ukiendelea nchi nzima, imeripoti SABC.
Wafanyakazi ambao hawatakuwepo kuhakikiwa wanahatarisha kutolipwa mshahara na ajira yao kusitishwa huku uchunguzi ukifanyika.
Mamlaka imesema malipo ya ulaghai kwa wafanyakazi hewa, ikiwemo kesi za kutumia namba za vitambulisho vinavyofanana, mishahara kulipwa kwa watu waliofariki, zinagharimu taifa mabilioni ya randi kila mwaka.
Kuweka akiba
Ukaguzi ni sehemu ya jitihada za kuokoa fedha zinazotumika kulipa fidia, ambazo ni takriban ya thuluthi moja ya matumizi ya serikali, kwa mujibu wa Hazina ya Taifa.
Sambamba na hilo, serikali imeanzisha mpango wa kustaafu mapema unaolenga kupunguza idadi ya wafanyakazi na kuokoa fedha.
Hazina imesema maombi 7,687 tayari yamepitishwa katika awamu ya kwa kwanza, ikitarajiwa kuokoa randi bilioni 2.6 katika mwaka wa fedha wa sasa.
Randi bilioni 3.7 pia zimetengwa kwa ajili ya mpango huo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na 2026/27.
Afrika Kusini imekuwa ikipambana na tatizo la wafanyakazi hewa kwa miaka kadhaa.
Mwaka 2025, kamati ya bunge ikishirikiana na Idara ya Utumishi wa Umma na Utawala, Mkaguzi Mkuu wa Afrika Kusini, na Hazina ya Taifa kutathmini ukubwa wa tatizo, wakielezea kama changamoto ya kitaifa ambayo inaongeza gharama, inamaliza rasilimali chache na kuondoa imani ya umma.
Tofauti na zoezi la awali la kuhesabu wafanyakazi, ukaguzi wa hivi karibuni umetegemea zaidi takwimu.
Hazina inakagua rekodi za mishahara dhidi ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini, utambulisho wa kutumia 'biometric' kutoka Idara ya Mambo ya Ndani, na taarifa za kibenki ili kubaini udanganyifu.
Maafisa wanasema zoezi hilo la uhakiki litaendelea kwa miezi kadhaa, huku hatua za kinidhamu na kihalifu zikitarajiwa dhidi ya kesi za ulaghai zilizothibitika.