Uturuki yasema kujiunga na EU haiwezekani katika mazingira ya sasa ya kisiasa

Mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki anasema mbinu ya Brussels imechangiwa na upendeleo wa kitamaduni na kidini, na kufanya uanachama wa Umoja wa Ulaya kutoweza kufikiwa licha ya maendeleo ya mahitaji ya kiufundi.

By
Picha ya faili ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan. / Reuters / Reuters

Uturuki haitaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya mpaka jumuia hiyo ipitie mabadiliko makubwa katika mtizamo wake wa kisiasa, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan Jumapili, akiiutuhumu EU kwa kuitenga Uturuki kwa misingi ya utambulisho, dini na ustaarabu.

Akizungumza katika mahojiano na Sky News Arabia, Fidan amesema licha ya kuwepo kwa maslahi ya pamoja kati ya Uturuki na EU, bado kuna kikwazo kikubwa kinachozuia maendeleo.

“Kadri Umoja wa Ulaya unavyoendelea na msimamo wake wa kisiasa dhidi ya Uturuki, siamini Uturuki itakuwa mwanachama wa EU," amesema Fidan, na kusisitiza kwamba mkwamo unatokana na mtazamo na fikra kuliko kutokubaliana kwa sera.

Siasa za utambulisho zaizuia Uturuki kuwa mwanachama

Fidan amesema kuwa msimamo wa EU kwa Uturuki unasababishwa na kile alichokiita “mtazamo wa utambulisho wa kisiasa," ambao, kwa maoni yake, inafanya ugumu kujiunga licha ya kufuata masharti yote rasmi.

Ingawa Uturuki imekuwa ikiwania rasmi nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka ishirini, majadiliano yamekuwa yakikwama kutokana na wasiwasi wa haki za binadamu, vigezo vya utawala, na migogoro ya kikanda.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, mkwamo huo unaonesha mkwamo wa kisiasa na kitamaduni, na EU ikiitathmini Uturuki kupitia vigezo ambavyo amesema kimsingi haviendani na utangamano wa kweli.

Akikosoa baadhi ya miradi ya EU, Fidan ametambua mafanikio ya Umoja wa Ulaya katika kuweka mfumo usio wa kawaida unaokwenda zaidi ya mamlaka ya nchi moja moja.

Hata hivyo, amesema kuwa mafanikio haya yameshindwa kukumbatia uhalisia wa tofauti za ustaarabu.

"EU iliweza kuwa taasisi iliyojipandisha juu ya kiwango cha kitaifa, lakini haikuweza kuwa taasisi inayozidi ustaarabu," alisema Fidan, akisisitiza kwamba kutengwa kwa Uturuki kunatokana na mtazamo wa tofauti za kidini na za ustaarabu.

Alielezea suala hilo kama la utambulisho badala ya vigezo vya kiufundi visivyotimizwa, akitaka kuonyesha kwamba mipaka ya kitamaduni, sio upungufu wa sera, ndiyo msingi wa kuahirishwa kwa ombi la uanachama wa Uturuki.

Utaratibu wa dunia unategemea ujumuishaji wa ustaarabu

Kwa kumalizia, Fidan aliunganisha kikwazo cha uanachama wa Uturuki katika EU na changamoto kubwa za kimataifa, akadai kuwa matatizo yanayokabili dunia hayawezi kutatuliwa kwa mbinu za kutenga watu pembeni. Badala yake, alitaka mifano jumuishi ya ushirikiano inayoleta pamoja ustaarabu tofauti.

Alipendekeza kwamba mustakabali wa binadamu unategemea uwezo wa ustaarabu mbalimbali kuishi pamoja chini ya mfumo wa pamoja, ukitaja kwa njia isiyo ya moja kwa moja ukosoaji wa jinsi EU, kwa maoni yake, haijafanikiwa kutimiza wazo hilo katika uhusiano wake na Uturuki.