Kardinali Pietro Parolin ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican amesema kuwa, taifa hilo halitoshiriki kwenye mkutano wa amani ulioandaliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, akiongeza kuwa jukumu la upatikanaji utulivu duniani ni la Umoja wa Mataifa.
"Suala ni moja tu, jukumu la kutatua migogoro ulimwenguni libaki kwa Umoja wa Mataifa. Hizi ni kati ya hoja tunazoziwasilisha, alisema Kardinali Parolin.
Hatua hiyo inakuja wakati Papa Leo wa 14, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani mwenye uraia wa Marekani alipoalikwa kwenye kikao hicho.
Mpango huo wa amani wa Trump unalenga kutatua migogoro ulimwenguni, huku yeye mwenyewe akiwa ndiye mwenyekiti wa bodi hiyo.
Bodi hiyo itakuwa na kikao chake cha kwanza jijini Washinton siku ya Alhamisi, ambapo watajadiliana ujenzi mpya wa Gaza.
Bodi hiyo ya Trump inaundwa na washirika wa Marekani walioko Ulaya, Mashariki ya Kati, Asia Mashariki na Marekani ya Kusini.
Kwa upande wao, Italia na Umoja wa Ulaya wametuma wawakilishi kama watazamaji tu, licha ya kutojiunga na bodi hiyo.
Mexico yakataa uanachama kamili
Wakati huo huo, Rais Clauida Sheinbaum alisema siku ya Jumanne kuwa, nchi yake haitoshiriki kama mwanachama kamili katika mchakato wa utafutaji amani Gaza, kutokana na kukosekana kwa uwakilishi wa Gaza katika bodi hiyo Trump.
“Kwakuwa tunaitambua Palestina kama taifa, ni muhimu kwa pande zote, Israel na Palestina zihusike kwenye mchakato huo,” alisema.
Kulingana na Sheinbaum, nchi yake itatuma balozi kwenda Umoja wa Mataifa kama mtazamaji tu.
“Walitupa mwaliko kama watazamaji; kama hatutoshiriki, basi tutakuwa watazamaji tu. Tuliamua kwa pamoja, kuwa balozi wetu wa Umoja wa Mataifa ahudhurie kama mtazamaji,” aliongeza.
Sheinbaum ameiunga mkono Palestina, akiyaita mashambulizi dhidi ya Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari.
















