Kenya: Vifo vilivyotokana na mafuriko vyafikia 50
Mamlaka za nchi hiyo zimeendelea kutuma vikosi vya uokoaji katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Vifo vilivyotokana na mafuriko nchini Kenya, sasa vimefikia 50, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema.
Jumla ya kaunti 17 zimeathirika na mafuriko hayo, hadi kufikia sasa.
Mamlaka nchini humo, zinasema kuwa watu tisa bado hawajulikani walipo huku nyumba 12, 338 zikiharibiwa na mafuriko hayo.
“Hadi sasa kaunti 17 zimeathirika na mafuriko haya huku tukitarajia hali kuwa mbaya zaidi, timu za uokoaji zipo timamu kuhakikisha zinatoa msaada wa kwa kaya zilizoathirika,” wizara hiyo ilisema.
Kati ya kaunti zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo ni pamoja na Nairobi, Kisumu, Narok, Kiambu, Migori, Siaya, Makueni, Busia, Wajir, Kisii, Homa Bay, Taita Taveta, Baringo, Kajiado, Kitui, Kwale na Machakos.
Mvua hizo, pia zimeharibu miundombinu kadhaa ikiwemo barabara, madaraja, njia za umeme pamoja na shule.