Afrika Kusini yazuia magari 60 baada ya ajali mbaya ya basi la shule
Polisi katika mkoa wa Gauteng wamethibitisha kuwa wanafunzi wawili wamefariki wakiwa hospitali siku ya Alhamisi, kufanya idadi ya waliofariki katika ajali kufikia 14.
Mamlaka nchini Afrika Kusini imezidisha msako unaozingatia masuala ya usalama ya usafiri wa shule katika mkoa wa Gauteng kufuatia ajali mbaya iliyosababisha vifo vya wanafunzi 14, huku magari mengine 60 yakizuiwa wakati wa operesheni hiyo huko Lenasia, kusini mwa mji wa Johannesburg.
Operesheni hiyo inakuja siku kadhaa baada ya gari moja lililokuwa likisafirisha wanafunzi kupata ajali eneo la Vanderbijlpark, mkoa wa Gauteng, siku ya Jumatatu. Polisi mkoa wa Gauteng walithibitisha kuwa wanafunzi wawili zaidi walifariki dunia hospitalini siku ya Alhamisi, kufanya idadi ya waliofariki kufikia 14.
Wakati wa operesheni ya siku ya Alhamisi, Idara ya Uchukuzi inasema mamlaka zimefanya ukaguzi wa magari kutathmini kama yanatimiza vigezo, ikiwemo hali yao ya usajili, viwango vya madereva, kujaza abiria kupita kiasi, na ubora wa magari.
“Walikuwa wanakagua magari ya shule kuona kama yanatimiza masharti, ikiwemo kuthibitisha usajili, tathmini ya kuona kama imejaza abiria kupita kiasi, dereva kutekeleza vigezo vya usalama barabarani, na kuangalia ubora wa magari. Magari ambayo hayafai kuwepo barabarani yatazuiliwa mara moja,” idara hiyo ilisema katika taarifa.
Msemaji wa polisi wa Mkoa, Mavela Masondo alisema dereva huyo wa shule mwenye umri wa miaka 22 aliyehusika katika ajali sasa anakabiliwa na mashtaka 14 ya mauaji, pamoja na kuendesha gari kiholela.