Jamhuri ya Congo yafanya Uchaguzi Mkuu
Rais wa sasa Denis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 82 anachuana na wagombea wengine sita.
Jamhuri ya Congo inafanya Uchaguzi wake Mkuu hii leo Machi 15, 2026, kumchagua rais.
Zoezi la kupiga kura lilianza saa moja asubuhi kwa saa za ndani (0600 GMT) na litakamilika saa kumi na mbili jioni.
Zaidi ya Wacongo milioni 3.2 wamejiandikisha kupiga kura.
Rais wa sasa Denis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 82 anachuana tena na iwapo atashinda basi itakuwa muhula wake wa tano mtawalia.
Kuna wagombea sita katika mchuano huyo, ingawa wachambuzi wanasema hakuna anayeonekana kuwa mpinzani mkubwa.
"Upinzani umegawanyika na hauna mtu madhubuti," alisema Remadji Hoinathy wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama yenye makao yake makuu mjini Pretoria. "Kunaweza kuwa na uchovu kati ya wapiga kura, lakini hiyo haitaathiri nafasi ya Sassou."
Viongozi wawili wa upinzani nchini humo wanasalia gerezani, huku wengine wakiwa uhamishoni.
Vyama kadhaa vya upinzani vimesusia uchaguzi huo, kwa madai mchakato huo hauendeshwi kwa usawa.
Sassou alichukua mamlaka ya nchi hiyo inayozalisha mafuta ya Afrika ya Kati mwaka 1979 na ametawala kwa mfululizo tangu wakati huo, isipokuwa kwa mapumziko ya miaka mitano katika miaka ya 1990.
Baadhi ya raia wa Congo wanasema wanaona nafasi ndogo ya mabadiliko.
Waziri Mkuu Anatole Collinet Makosso amepuuzilia mbali shutuma za kuegemea upande wa Sassou, akisema kuwa vyombo vya uangalizi vya Congo vitahakikisha uchaguzi unakuwa wa wazi na wa haki.
Sassou amefanya kampeni akiahidi kuharakisha miradi ya maendeleo na kupanua upatikanaji wa elimu na mafunzo ya kitaaluma.
Uchumi wa Congo unaotegemea sana mafuta, umetulia katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuzorota kwa muda mrefu, lakini asilimia 52 ya watu milioni 6.1 wa Congo wanaishi katika umaskini, kulingana na Benki ya Dunia.
Matokeo ya muda ya uchaguzi yanatarajiwa kutoka kati ya saa 48 hadi 72 baada ya upigaji kura kufungwa.