Watu watano wafariki katika ajali ya helikopta nchini Libya

Helikopta hiyo ilianguka katika kambi ya al-Sarra baada ya zoezi la uokoaji kutoka Kufra.

By
Helikopta hiyo imepata ajali katika kambi ya al-Sarra. / Reuters / Reuters

Helikopta ya wagonjwa imepata ajali ilipokuwa inashuka katika kambi ya Al-Sarra nchini Libya, na kuuwa watu watano, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Ajali hiyo imetokea siku ya Jumatatu, takriban kilomita 300 (maili 186) kutoka mji wa Kufra uliopo kusini mashariki, kwa mujibu wa chombo cha habari cha al-Wasat, kikinukuu vyanzo vyenye taarifa.

Waliofariki ni pamoja na wanajeshi wawili kutoka kitengo cha usafirishaji, pamoja na muuguzi kutoka hospitali ya Kufra.

Wawili wengine walikuwa ni raia wa kigeni, wakitambulika kama rubani na msaidizi wake, taarifa hiyo imesema.

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa mara moja kuhusu chanzo cha ajali, na mamlaka nchini Libya bado hazijatoa taarifa rasmi ya ajali.

Zoezi la uokoaji

Kwa mujibu wa taarifa ya Aviation Today, helikopta hiyo ya jeshi ilikuwa katika zoezi la uokoaji baada ya mwanajeshi mmoja kujeruhiwa katika ajali ya barabarani katika eneo la jangwani karibu na Kufra.

Taarifa imeongeza kusema kuwa, vikosi vya dharura vilifika haraka katika eneo la ajali, na kuthibitisha kwamba hakuna aliyepona katika ajali hiyo.