Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imemteua Balozi Olara Otunnu kugombea nafasi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
"Serikali ya Uganda imemteua na kuwasilisha maombi ya Balozi Olara Otunnu, mwanasiasa mahiri na mtumishi wa umma wa kimataifa, kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa," imesema taaifa hiyo iliyotolewa Julai 26, 2026 na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara Bagiire Vincent Waiswa.
Taarifa hiyo pia imetaja uzoefu aliokuwa nao Balozi Otunnu katika nyanja za kimataifa.
Mpaka sasa, Otunnu atakuwa ni mgombea wa pili kutoka Afrika, baada ya rais wa zamani wa Senegal Macky Sall nae kuingia katika kinyang'anyiro hicho.
Hii inafanya idadi ya wagombea wanaotaka kumrithi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kufikia 6.
Guterres anamaliza muhula wake Disemba 31, 2026.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump amempigia chapuo rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA), Gianni Infantino na kumtaka aingie katika kinyang'anyiro hicho.










