Amani ya kudumu vita vya Urusi-Ukraine 'iko karibu':Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki
Hakan Fidan ameeleza kuwa Uturuki "itachukua jukumu la kuimarisha ulinzi wa eneo la baharini pale amani itakapopatikana".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan anasema kufikiwa kwa amani ya kudumu katika vita vya Urusi na Ukraine sasa "kuko karibu".
“Kwa maoni yangu, baada ya miaka minne ya vita, sasa hivi tuko karibu kufikia amani ya kudumu. Kwa uchache, tunaona maeneo kadhaa ambayo ni muhimu kwa upatikanaji wa amani yanajadiliwa kwa uzito zaidi," Fidan amewaambia waandishi wa habari katika Ubalozi wa Uturuki mjini Paris siku ya Jumanne baada ya mkutano wa Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Ukraine.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa mkutano wa Paris, Fidan alisema alimwakilisha Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano huo, ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wa mataifa na taasisi kama vile EU na NATO. "Masuala muhimu yalijadiliwa," alisema.
"Tunachokiona ni kuwa, yakitiwa saini, haya hayatokuwa makubaliano tu ya amani yatakayomaliza vita nchini Ukraine. Yatatoa muelekeo ya muda mrefu, ya namna amani itakavyokuwa kati ya Urusi na Ulaya kwa ujumla. Wakati huo huo, yatakuwa ya masuala kadhaa ambayo yataangazia sera ya Urusi katika kanda," waziri huyo wa mambo ya nje wa Uturuki aliongeza.
'Ni suala la msingi kwa Uturuki kuwa na jukumu la usalama katika Bahari Nyeusi'
Fidan alisema uwezekano wa kusitishwa mapigano, kuzuia Ukraine, na uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi pale usitishwaji wa mapigano utakapokiukwa yalikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa.
“Kuanzia mwanzo, chini ya maagizo ya rais wetu, jeshi letu limekuwa na msimamo kuwa litakuwa na jukumu la ulinzi wa baharini pale amani itakapopatikana. Naamini hatua za msingi zimepigwa kuhusu hili.
"Ukizingatia kuwa Uturuki ni mwanachama wa NATO aliye na idadi kubwa ya vyombo katika Bahari Nyeusi, ni suala la msingi kwa Uturuki kuwa na jukumu la Usalama katika Bahari Nyeusi ... Ni matarajio yetu, kuwa makubaliano ya amani yatatiwa saini hivi karibuni, ili kuepusha vifo zaidi na kuleta usalama katika kanda hiyo," alieleza zaidi.
Fidan alisema kuwa katika kikao kingine siku ya Jumanne kiliangazia kufufua uchumi wa Ukraine iwapo makubaliano ya amani yatatiwa saini.
Alisisitiza kuhusu umuhimu aliouweka Rais Erdogan kuhusu suala hilo na kusema kuwa hakuna nchi "yenye uwezo zaidi ya Uturuki linapokuja suala la kuponya vidonda."
"Tuko vizuri katika uponyaji wa vidonda na kwa wale watu wanaohitaji misaada. Uwekezaji wa kiuchumi na utaalamu wa wafanyabiashara wetu, hasa katika miundombinu, ni muhimu sana. Tunaamini pindi amani itakapopatikana, Uturuki itakuwa na jukumu muhimu la kufufua uchumi na maendeleo,” aliongeza.
Fidan alisema pia alikuwa na mikutano na wakuu wa nchi, kujadili masuala muhimu, na kufanya tathmini ya kuhusu agenda hiyo na maafisa wa Umoja wa Ulaya.
Mashambulizi ya Israel nchini Syria ‘ni uchokozi’
Fidan aliongeza kuwa pia walijadili masuala kadhaa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al Shaibani, ambaye alikuwepo Paris kwa mkutano mwingine wa utatu pamoja na Marekani na Israel. Aliongeza kuwa Uturuki inaendelea kufuatilia mazungumzo ya pande hizo tatu.
“Kila mara tunawasiliana na wote Syria na Marekani. Baada ya mazungumzo hayo, tulikutana naye. Tulipata fursa ya kujadili kwa kina masuala kadhaa — walipofikia hadi sasa katika majadiliano na matokeo yake, au kutokuwepo kwa yote hayo, kuhusu mazungumzo waliyofanya na YPG siku chache zilizopita. Tulipitia masuala yote kwa makini sana,” Fidan alisema.
YPG ni tawi la Syria la kundi la kigaidi la PKK.
Fidan pia alikutana na Balozi wa Marekani nchini Uturuki na Mjumbe Maalum wa Syria Tom Barrack, akiongeza kuwa alifahamishwa kuhusu mazungumzo ya utatu na akatoa maoni yake.
Jeshi la Israel limeshambulia mara kadhaa ndani ya Syria tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al Assad mwishoni mwa 2024, mashambulizi ambayo Syria yameshtumu vikali.
Kuyataja mashambulizi ya Israel nchini Syria "uchochezi," Fidan amesema yalikuwa "sehemu ya sera za upanuzi za Israel na kuleta mgawanyiko katika mipaka ya kanda.
"Tunaona wazi. Ni muhimu sana kwa usalama wa kanda kwamba tathmini muhimu ifanyike, idadavuliwe, na hatua muafaka zichukuliwe."
Fidan alisema nchi katika kanda lazima ziangalie suala hili, akisisitiza kuwa Marekani inaweza kuwa na jukumu muhimu katika hili.
Israel kutambua Somaliland ishara ya 'kutozingatia uhalali'
Kuhusu hatua ya Israel ya hivi karibuni kutambua eneo lililojitenga la Somalia, Somaliland,na kusababisha kushtumiwa kimataifa, Fidan amesema hii ni moja ya miradi ya Israel ya kusababisha ukosefu wa usalama katika kanda.
Mapema siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar alifanya ziara Somaliland tarkriban wiki mbili baada ya uamuzi wa kutambua eneo hilo kama taifa tofauti.
"Tumesema wazi hatua ambazo zinalenga kugawanya mipaka ya nchi huru kwa njia hii haikubaliki, hilo ‘linagawanya, kusambaratisha, na kuzima au kutawala kwa ‘ mfumo wa sera kama hizi katika kanda ni jambo lililopitwa na wakati, na kwamba nchi katika kanda, zikishirikiana, hazitoruhusu hili kufanyika," alisema.
Fidan pia alieleza kuhusu matatizo ya muda mrefu kati ya Somaliland na serikali ya Somalia na kusema kuwa balozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki amepewa jukumu la upatanisho katika suala hilo.
“Hata hivyo, kwa misingi ya miongozo ya Umoja wa Mataifa, sera zetu wenyewe, na utaratibu wa kimataifa, tumekuwa daima tukitetea uhuru wa mipaka ya Somalia. Tumekuwa tunatarajia kuwa watatatua masuala yao ya ndani kwa amani," alisema.
Fidan alieleza kuwa kwa Israel kutambua Somaliland ni ishara ya "kutozingatia uhalali." "Kuna tofauti gani kwa nchi kama Israel, ambayo yenyewe uhalali wake unatiliwa shaka, kuunga mkono Somaliland? ... Tunaona kama ni hatua ya kimkakati, ya kuonesha uwezo wake."