Serikali ya Kenya imetangaza kutoa msamaha wa kodi katika ujenzi wa mradi wa kiwanda cha Dangote cha kusafisha mafuta, unaofanyika huko Lamu, pwani ya Kenya.
Waziri wa Fedha wa nchi hiyo John Mbadi anasema msamaha huo utakuwa katika bidhaa za mitaji zinazoletwa nchini kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, ikiwa ni pamoja na Ushuru wa Thamani (VAT), ushuru wa bidhaa, na ushuru wa maendeleo ya reli.
Mbadi alitoa taarifa hiyo wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen TV, chenye makao yake jijini Nairobi, mnamo Jumanne jioni.
Mbadi amesema kuwa uwekezaji huo unastahili kupata motisha chini ya sheria ya Kenya, ambayo hutoa msamaha wa kodi kwa miradi yenye uwekezaji wa mitaji unaozidi zaidi ya Dola milioni 38 (shilingi 5 bilioni).
"Bidhaa zozote za mtaji watakazoleta zitastahiki kupata msamaha wa kodi kama ilivyo kwa nyinginezo, na kutakuwa na utaratibu rasmi wa kuwasilisha ombi," alisema Mbadi.
Kiwanda hicho kilichopendekezwa cha kusafisha mafuta kinakadiriwa kugharimu takriban dola bilioni 16 (Ksh2 trilioni) na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusindika mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kila siku mara tu kitakapokamilika.
Kulingana na taarifa alizotoa katika mahojiano hayo, Waziri Mbadi ameongeza kusema kuwa Dangote tayari alikuwa amelipia kodi baadhi ya vifaa vilivyoagizwa ili kuanza mradi huo lakini ataruhusiwa kudai marejesho baada ya kuwasilisha maombi rasmi.
Hata hivyo, Mbadi alihakikisha kuwa kampuni hiyo itarejeshewa fedha zake.
"Lazima wawe wamelipa," alisema Mbadi. "Kisha watawasilisha madai, nasi tutawapa fedha hizo."





















