Kwa nini ushirikiano wa Somalia na Uturuki unaimarika licha ya minong'ono
Uimara wa ushirikiano wa Somalia na Uturuki umejikita zaidi kwenye matokeo. Ni ushirikiano uliojengwa kwa msingi wa kuaminiana, umekuwepo kwa muda mrefu, na mafanikio yake yanaonekana.
Na Balozi Fathudin Ali Ospite
Ushirikiano kati ya Serikali ya Somalia na ile ya Jamhuri ya Uturuki ni moja kati ya ushirikiano muhimu na wenye tija kwa mataifa haya mawili kimataifa.
Katika kipindi ambacho simulizi zinaweza kusambaa kuliko ukweli na kupindisha uhalisia, ushirikiano huu unajitokeza kuwa tofauti, ukidhihirisha heshima, na matokeo yenye tija.
Pamoja na kuwa umekuwa ukiangaziwa kwa makini —na wakati mwingine kukosolewa - uimara wake uko kwenye uwezo wake wa kushinda minong’ono kupitia hali endelevu, uwazi, na malengo ya pamoja.
Nakumbuka kuhusu tukio moja la ucheshi lakini lenye ujumbe mzito kati ya Waziri wa Mazingira wa Somalia Mheshimiwa Bashir Mohamed Jama, na mwenzake wa Uturuki, Mheshimiwa Murat Kurum. Alipoulizwa kuhusu idadi ya watu wa Somalia, Waziri Jama alijibu: “Watu milioni 105, ukichanganya Waturuki milioni 85 na Wasomali milioni 20.”
Mbali na ucheshi huo kuna ukweli ndani yake: ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili ni zaidi ya itifaki au sera. Umejengwa kwa misingi ya maadili na umoja—ambapo Waturuki na Wasomali hawatizamani kama washirika wa mbali, lakini kama familia moja.
Wakati nikielekea kukamilisha miaka miwili ya Ubalozi, naangazia kuhusu miezi yangu ishirini na miwili ya kujumuika, majadiliano, na kujifunza. Hali hii imeimarisha fikra zangu kuhusu ushirikiano wa Somalia na Uturuki siyo tu unaleta tija, bali unaleta mabadiliko.
Wakati muhimu
Chimbuko la ushirikiano huu limeanza enzi za wakati muhimu katika historia ya Somalia, kipindi Uturuki ilipoamua kujihusisha wazi wakati jamii ya kimataifa ikijitenga. Kile kilichoanza kama kuwaunga mkono kikachanga kuwepo kwa ushirikiano katika sekta muhimu za ujenzi upya wa Somalia na maendeleo ya muda mrefu —yanayoongozwa na lengo la pamoja mafanikio endelevu.
Leo hii, ushirikiano huo uko katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo afya, ulinzi na usalama, miundombinu, nishati, elimu, na uimarishaji wa taasisi. Haya ni misingi ya kuimarisha Somalia na mabadiliko ya kiuchumi.
Maeneo ya mafunzo ya kijeshi ya Uturuki mjini Mogadishu, kwa mfano, yanawakilisha zaidi ya ushirikiano wa kiusalama —ni uwekezaji wa muda mrefu kwa uwezo wa Somalia kujenga na kuimarisha taasisi zake wenyewe za taifa. Vile vile, ushirikiano katika serkta za uchumi unaotokana na bahari unaashiria kutambuliwa kwa Somalia kama sehemu ya kimkakati na yenye uwezo mkubwa kiuchumi.
Ushirikiano huu umejengwa kwa misingi ya kuhusisha pande zote na heshima kwa uhuru wa nchi. Hili linaonekana wazi katika ushirikiano wa kila siku miongoni mwa wasomi wa Somalia na Uturuki katika sekta mbalimbali. Kuanzia uimarishaji wa miundombinu hadi katika masuala ya afya na elimu, ushirikiano huu unaendelea kuleta matokeo muhimu na yenye tija.
Somalia, kama nchi nyingine ile inayopitia mabadiliko ya kisiasa, inakabiliwa na changamoto ambazo zinatakiwa kutatuliwa nyumbani. Tofauti za kisiasa ni sehemu ya kukuwa kwa demokrasia. Hata hivyo, kulaumu changamoto hizi kwa washirika wa nje kunahatarisha kutotambua suala lenyewe na kutozingatia ushirikiano ambao ni muhimu kwa kuimarika kwa taifa.
Juhudi za kuingiza siasa au kushusha hadhi ya ushirikiano huo zinashindwa kutoa ufafanuzi kuhusu uweledi wake, mafanikio yake, na faida kwa pande zote mbili.
Matokeo yake yako wazi. Uwekezaji katika miundombinu, sekta ya afya, na elimu yameimarisha huduma za umma, fursa za kiuchumi, na kuwa na faida zinazoonekana kwa raia wa Somalia. Matokeo haya yanaonesha namna gani mifumo mizuri ya ushirikiano wa kimataifa inavyoweza kuimarisha maisha ya watu.
Uwezo wa ushirikiano wa Somalia na Uturuki umejikita zaidi katika kuwa na matokeo. Ni ushirikiano uliojengwa katika misingi ya kuaminiana, umekuwepo kwa muda mrefu, na mafaniko yake yanaonekana. Huku kukiwa na minong’ono, unaendelea kusimama imara-ukiongozwa kwa dhamia ya pamoja ya maadili, kuheshimiana, na dira moja ya kuwa na mustakabali salama na wenye mafanikio.
Mwandishi, Balozi Fathudin Ali Ospite, ni Balozi wa Jamhuri ya Somalia katika Jamhuri ya Uturuki.