Kwa muda mrefu sasa, mjadala wa kupata simulizi za Afrika umekosa muafaka.
Hata hivyo, Moky Makura anadhani kuna mengi ya kufanya kufikia mafanikio.
Makura, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ‘Africa No Filter’, na wenzake, wametumia miaka sita kutengeneza nyenzo za kuleta mabadiliko.
Kwa pamoja, wametengeneza kamusi maalumu, yenye kutumia Akili Mnemba, maalumu kwa waandishi wa habari, ili waweze kubaini namna wanavyoripoti kazi zao bila upendeleo.
"Tunajaribu kubadili mtazamo wa watu kuhusu Afrika," anasema Makura katika mahojiano na TRT Afrika.
"Hii ni kamusi yenye kuzungumza lugha ya kiafrika."
Anasema kuwa, timu yake inatumia nyenzo hiyo, kuwajengea uwezo wengine.
Makura ana imani kuwa, nyenzo hiyo itawasaidia waandishi wa habari, mashirika ya maendeleo na wataalamu wa mawasiliano, kutengeneza vichwa vya habari visivyo na utata.
Hivi karibuni, taasisi hiyo, ilizindua nyenzo ya uhariri yenye kutumia teknolojia ya Akili Mnemba, yenye uwezo wa kupitia taarifa kabla ya kuandikwa na kuchapishwa.
"Nyenzo hii haikusaidii kuandaa taarifa bali inakusaidia kuanisha maeneo tata kwenye taarifa hizo, " anaeleza.
Utafiti ulioandaliwa na taasisi hiyo, unaweka bayana gharama za kuripoti taarifa za Afrika kwa njia zenye utata.
Taasisi hiyo, inadai kuwa, serikali nyingi za Afrika, zinajikuta zikilipa Dola bilioni 4.2 kwa mwaka, kukabiliana na hali hiyo.
Hoja hiyo, inaungwa mkono na Umoja wa Afrika, mashirika ya maendeleo na wataalamu wa fedha, wanaosema kuwa Afrika inaingia gharama kubwa kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake, Umoja wa Afrika umelipa suala hilo kipaumbele maalumu, kupitia Ajenda ya mwaka 2063, kwa kutumia majukwaa mbalimbali kama vile vyombo vya habari barani Afrika.
Hata hivyo, Makura anasisitiza kuwa, si vyema jukumu hilo, likaachiwa serikali, taasisi na vyombo vya habari peke yao.
Badala ya kuwauliza watu simulizi nzuri, kampeni hii huuliza watu maswali binafsi.
"Huwa tunauliza watu wamefanya nini, bila kufanya hivyo, hakuna kinachoweza kuonekana,” anasema Makura.
Kampeni hiyo, inaunga mkono jitahada za Waafrika kuzungumzia simulizi zao, kupitia jamii zao na biashara zao, kwani simulizi hizo huwa hazipewi nafasi.
"Tunachofanya kwa sasa, ni kuangazia yale ambayo tayari yameshafanyika," anasema.
Makura anaamini kuwa, Waafrika waishio ughaibuni wana nafasi katika jambo hilo.
Makura anaamini kuwa, Waafrika waishio ughaibuni wana nafasi katika jambo hilo.
"Nadhani tuna faida kubwa, kwani tumetawanyika mahali mbalimbali," anaeleza.
“Wenzetu waishio ughaibuni wana nafasi kubwa ya kufikisha simulizi zetu kimataifa, lakini pia kuwekeza nyumbani."
Kupitia kampeni yake ya Africa No Filter, kubadilisha mtazamo kuhusu Afrika, kunahitaji kushirikisha kila mtu.
“Kwa sababu wakati dunia inapoendelea kujadili mustakabali wa Afrika, mamilioni wa Afrika wanaendelea kulijenga bara lao,”anasema Makara.















