| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mbu aliyeletwa na ndege Ujerumani asababisha vifo vya watu wawili
Mamlaka ya afya ya jiji la Frankfurt ilithibitisha vifo hivyo Jumatano.
Mbu aliyeletwa na ndege Ujerumani asababisha vifo vya watu wawili
mitego maalumu ya kuwanasa mbu imewekwa katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo ili kudhibiti uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo. / / Reuters

Wafanyakazi wawili katika Uwanja wa Ndege wa Frankfurt nchini Ujerumani wamefariki dunia baada ya kuambukizwa malaria, ugonjwa unaodhaniwa kusababishwa na mbu aliyeingia nchini humo kupitia ndege ya abiria.

Mamlaka ya afya ya jiji la Frankfurt ilithibitisha vifo hivyo Jumatano.

Awali, maafisa wa uwanja huo walikuwa wametangaza kuwa mfanyakazi mmoja amefariki dunia na kwamba wafanyakazi wengine sita walikuwa wameambukizwa malaria.

Taasisi ya Robert Koch (RKI), inayohusika na masuala ya afya ya umma nchini Ujerumani, imesema kuna uwezekano mkubwa kuwa malaria hiyo ilisababishwa na mbu aina ya Anopheles aliyeletwa nchini humo kupitia ndege ya abiria iliyoingia nchini humo.

Msemaji wa uwanja wa ndege amesema wafanyakazi wengine wanne waliokuwa wameambukizwa wanaendelea kupata matibabu hospitalini.

Aidha, mitego maalumu ya kuwanasa mbu imewekwa katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo ili kudhibiti uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa RKI, mlipuko wa mwisho wa malaria unaohusishwa na uwanja wa ndege nchini Ujerumani uliripotiwa mwaka 2023.

Hata hivyo, maambukizi ya aina hii ni nadra nchini humo, hali ambayo inaweza kufanya utambuzi wa ugonjwa kuchelewa na kuongeza hatari ya wagonjwa kupata dalili kali za ugonjwa huo.

Taasisi ya Tropical Medicine ya nchini Ubelgiji imepewa jukumu la kuchunguza vimelea vya malaria vilivyopatikana katika sampuli za damu za wagonjwa.

Malaria husababishwa na vimelea vinavyoenezwa kwa kuumwa na mbu aina ya Anopheles.

Dalili zake zinaweza kujumuisha kichefuchefu, maumivu ya kichwa, homa kali pamoja na kutetemeka na kuhisi baridi.

Ugonjwa wa malaria husababisha mamia ya maelfu ya vifo kila mwaka, huku idadi kubwa ya waathirika ikiwa katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hata hivyo, matibabu ya malaria yanapatikana, na wagonjwa wanaogundulika na kuanza matibabu mapema kwa kawaida hupona kikamilifu.

 

CHANZO:AFP