AU yataka kusitishwa kwa mapigano katika jimbo la Jonglei, Sudan Kusini
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amekana madai kwamba serikali inawalenga raia.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ametaka kusitishwa mara moja kwa mgogoro unaoendelea Sudan Kusini na kutaka kuheshimiwa kwa makubaliano ya Sudan Kusini ya Amani ya mwaka 2018, wakati ambapo mapigano mapya katika jimbo la Jonglei yamesababisha zaidi ya watu 180,000 kukimbia makazi yao hivyo kuibua taharuki miongoni mwa raia.
Katika taarifa yake, mwenyekiti wa Tume ya AU Mahmoud Ali Youssouf ameonesha wasiwasi wake kufuatia kudorora kwa hali ya usalama katika maeneo ya nchi, hasa Jonglei, ambapo kuongezeka kwa vurugu na matamshi ya uchochezi kumewaweka wananchi, hasa watoto na wanawake katika hali ya hatari.
Serikali ya Sudan Kusini inakisia idadi ya waliohama makazi yao katika jimbo la Jonglei kufikia 180,000, hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu OCHA.
“Mwenyekiti ana wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za matamshi ya uchochezi na vitendo ambavyo vinahatarisha kuongezeka kwa mgogoro na kuhatarisha maisha ya watu ikiwemo watoto na wanawake," imesema taarifa hiyo.
Youssouf ametahadharisha kwamba vitendo hivyo vinaenda kinyume na makubaliano ya kutatua mgogoro katika Jamhuri ya Sudan Kusini na kulaani vitendo vya vurugu dhidi ya wananchi.
Kupunguza hali ya wasiwasi
Amezitaka pande zote kuwa na utulivu, na kupunguza hali ya wasiwasi haraka, na kufuata makubaliano ya kudumu ya usitishaji wa mapigano, na ushirikishwaji wa mamlaka kama ilivyo katika makubaliano.
“Ulinzi kwa raia bado ni kipaombele kwa pande zote,” taarifa hiyo imesema, na kuongeza kuwa AU itaendelea kufanya kazi na IGAD, UN, na washirika wa kimataifa kuunga mkono jitihada za kuleta amani na suluhu ya kitaifa nchini Sudan Kusini.
Wito huo unafuatia tangazo la Jeshi la Sudan Kusini SSPDF likiwataka wananchi, mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu, na watumishi wa Umoja wa Mataifa kuondoka maeneo ya Jonglei ambayo yamekaliwa na upinzani kabla ya kufanyika kwa oparesheni kubwa ya kijeshi.