Familia za waathirika 32 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya shirika la Ethiopia, wanatarajia kupokea kifuta machozi cha Dola milioni 87.3, miaka saba baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Kulingana na mawakili kutoka kampuni ya wanasheria ya Ribbeck Law, kampuni ya ndege Boeing imeanza kufanya mchakato wa malipo hayo, mara baada ya kumalizika kwa shauri la kisheria nchini Marekani.
Familia za waathiriwa hao, zinatarajiwa kulipwa kiasi cha Dola milioni 87,343,352.60, ambayo ni wastani wa Dola milioni 2.73 kwa kila aliyepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea mwaka 2019.
“Kwa sasa, tumekamilisha shauri lote la kisheria kwa niaba ya wateja wetu waliopo Marekani, Afrika, Mashariki ya Kati na Asia,” alisema mwakilishi wa kampuni hiyo, Manuel von Ribbeck.
Malipo hayo yanatokana na mfuko maalumu wa fidia wa dola milioni 444.5 ulioanzishwa na Idara ya Haki ya Marekani (DoJ) kufuatia makubaliano na kampuni ya ndege ya Boeing.
Ndege hiyo, aina ya Boeing 737 MAX, iliyokuwa ikieleka Nairobi, Kenya kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia, ilipata ajali Machi 10, 2019.
Jumla ya watu 149 walipoteza maisha katika ajali hiyo, wakiwemo raia 32 kutoka Kenya.



















