Raia wa Marekani anayefanya kazi katika shirika la kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amepimwa na kukutwa na virusi vya Ebola vya Bundibugyo, CDC ya Marekani ilisema Ijumaa.
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vinashirikiana na shirika lililomuajiri mgonjwa huyo, mashirika mengine ya shirikisho na washirika nchini DRC ili kusaidia kuzuia maambukizi zaidi na kutambua watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa, ilisema.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani siku ya Jumamosi alisema shirika hilo lilikuwa linajua kuhusu maambukizi hayo na lilikuwa likifanya kazi ya kumsaidia Mmarekani aliyeathiriwa. Msemaji huyo alikataa kutoa maelezo zaidi.
Bado haijabainika ni hatua gani Marekani itachukua ili kumhamisha mfanyakazi aliyeathiriwa kwa matibabu zaidi.
Pendekezo lilikataliwa
Marekani ilikuwa imependekeza kituo cha Ebola nchini Kenya ili kuwahudumia raia wake walio hatarini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.
Pendekezo hilo lilizuiwa kwa muda na Mahakama baada ya Wakenya kulikataa wakisema linahatarisha kuiweka nchi katika hatari ya mlipuko unaoendelea.
Ingawa mamlaka ya Kenya mwanzoni iliendelea na ujenzi wa kituo hicho, mahakama kuu ilikihukumu kusitishwa kwa muda na kuamuru Waziri wa Afya wa nchi hiyo Aden Duale kufika mbele yake kujibu madai ya kudharau mahakama.
Baadaye Duale aliomba msamaha kwa mahakama na kusimamisha ujenzi wa kituo hicho.
Aina ya Ebola ya Bundiggyo inayoenea nchini DRC kwa sasa haina chanjo au tiba inayojulikana ingawa wataalamu wa afya wameanza kutumia baadhi ya tiba ya majaribio ili kuidhibiti.
Hadi sasa watu 648 wamefariki kutokana na virusi vya Bundibugyo huku 1830 wakiwa wameambukizwa na angalau watu 300 wametibiwa kwa mafanikio.



















