Raia mmoja wa China amekamatwa akiwa na zaidi ya mchwa hai 2,200 kwenye mizigo yake alipokuwa akijaribu kuwapitisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Zhang Kequn, 27, alikamatwa Machi 10, 2026 alipokuwa akijaribu kuondoka nchini, hii ni kulingana na majalada ya mahakama yaliyoonekana na Reuters siku ya Alhamisi.
Maafisa wa uhamiaji waliripoti ilani ya tahadhari kwenye hati ya kusafiria ya Zhang baada ya kukwepa kukamatwa nchini Kenya mwaka jana.
Walanguzi wa siafu na mchwa hulipa kiasi kikubwa kudumisha makoloni katika vyombo vikubwa vya uwazi vinavyojulikana kama “formicariums,” ambapo huwatazama kama sehemu ya starehe.
Wanunuzi wengi wa wadudu na wanyama wa starehe wako Ulaya na Asia.
Mwaka jana washtakiwa wanne walitozwa faini ya dola 7,700 kila mmoja kwa kujaribu kusafirisha maelfu ya mchwa.
Ikiwa juhudu za kumaliza uharamia wa wadudu zimepewa kipaumbele nchini, uchunguzi zaidi umebaini sio tu pembe za ndovu zinazohamishwa, lakini pia aina nyengine ya wanyama na wadudu ambao ni kinyume cha sheria kusafirishwa.
Wachunguzi walisema upekuzi kwenye mizigo ya Zhang ulipata mchwa 2,238, wakiwemo 1,948 waliokuwa wamepakiwa ndani ya mirija na iliyobaki katika safu tatu za "karatasi laini za tishu."
Walisema Zhang alikuwa nchini Kenya kwa wiki mbili na wametaja washirika watatu ambao
walimpa mchwa hao.
Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya limepewa muda zaidi na mahakama ili kukamilisha uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuchunguza simu na kompyuta ya mtuhumiwa.
Huduma ya wanyamapori imesema shehena kama hiyo ya mchwa imekamatwa huko Bangkok siku ya Jumanne ikitokea Kenya, hali inayoonesha kuongezeka kwa biashara hiyo ya magendo.












