Kenya yapendekeza marufuku ya suluhu za nje ya mahakama kwa kesi za ubakaji
Kamati ya kiufundi ilibainisha kuwa suluhu za nje ya mahakama mara nyingi hufuatia shinikizo la kijamii badala ya usalama na utu wa waathirika.
Kamati ya kukabiliana na Unyanyasaji wa Kijinsia nchini Kenya imependekeza kupigwa marufuku kwa suluhu za nje ya mahakama kwa wahusika wa ubakaji na uhalifu mwingine wa Kijinsia.
Kikundi Kazi cha Kitaalam cha Ukatili wa Kijinsia (GBV) kimependekeza kufanyiwa marekebisho sheria ya makosa ya kingono kwa lengo la kukomesha ukwepaji adhabu na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathirika.
Katika ripoti yake kwa Rais William Ruto, Kamati hiyo imesema suluhu za nje ya mahakama zinahujumu utawala wa sheria.
‘’Kesi nyingi za unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa kijinsia, na mauaji ya wanawake mara kwa mara hutatuliwa nje ya mfumo rasmi wa haki kupitia mazungumzo ya kifamilia, wazee wa jamii, au utozaji fidia, utaratibu unaodhoofisha utawala wa sheria na kukiuka haki za kikatiba za wahanga,’’ ilisema ripoti hiyo.
Akipokea ripoti hiyo katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema waliopewa dhamana ya uongozi lazima wawalinde walio hatarini katika jamii.
‘’Viongozi wa kidini na viongozi wa jamii lazima wasimame kidete kutetea uhai na utu wa binadamu na lazima wakabiliane na mila potofu na kutokomeza ukimya unaolinda dhuluma,’’ alisema Rais Ruto.
Kikosi kazi hicho kiliitaka serikali kufanyia marekebisho sheria za kitaifa ili kuzuia suluhu zisizo rasmi, za kimila au makubaliano ya faragha kwa kesi za jinai za Ukatili wa Kijinsia, wakidai kuwa vitendo hivyo vimewafanya wahalifu kukwepa uwajibikaji huku wakiwanyamazisha waathirika.
Kamati ya kiufundi ilibainisha kuwa suluhu za nje ya mahakama mara nyingi hutanguliza shinikizo la kijamii badala ya usalama na utu wa waathirika.
‘’Waathiriwa, hasa wanawake na wasichana, mara nyingi wanalazimishwa kukubali suluhu kutokana na unyanyapaa, utegemezi wa kiuchumi, au woga wa kulipiza kisasi,’’ inasema ripoti hiyo.
Rais Ruto alisema mapendekezo hayo yatafikishwa kwa Baraza la Mawaziri, Bunge na taasisi husika za serikali. Pale ambapo marekebisho ya sheria yanahitajika, yatashughulikiwa kupitia taratibu za kikatiba zilizowekwa.
Kulingana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya na ripoti za serikali, zaidi ya kesi 31,000 za unyanyasaji wa kingono na kijinsia ziliwasilishwa katika mahakama za Kenya kati ya 2004 na 2005.
Takwimu za kihistoria za polisi pia zinaonesha takriban asilimia 92 ya unyanyasaji huo ulioripotiwa ulikuwa dhidi ya wanawake.
Polisi pia wanasema kwamba idadi kubwa bado haiwakilishi uhalisia wa uhalifu kwani kesi nyingi zaidi haziripotiwi.