Serikali ya Tanzania imeanza kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa upatikanaji wa mafuta nchini kwa kuunda timu maalum itakayohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mafuta yanafika nchini kwa wakati na kusambazwa bila usumbufu.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi akizungumza kutokea Dodoma, amesema changamoto kubwa katika sekta ya mafuta duniani si bei, bali ni upatikanaji wa mafuta ghafi, jambo ambalo linaathiri nchi nyingi ikiwemo Tanzania.
Ameeleza kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wananchi hawakosi mafuta, hasa kwa kuwa yanapatikana kwenye maghala lakini wakati mwingine hayafikishwi kwa walaji kwa haraka.
Waziri huyo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuongeza uangalizi ili kuzuia wafanyabiashara kuficha mafuta kwa lengo la kusubiri kupanda kwa bei.
Aidha, amesisitiza kuwa mafuta yaliyothibitishwa yaanze kusambazwa mara moja kuanzia bandari ya Dar es Salaam hadi maeneo ya ndani kama Kyelwa.
Katika kuhakikisha uwazi na ufuatiliaji, Wizara imeelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushirikiana kwa karibu na EWURA katika kuhakiki mafuta yote yanayoingia nchini kabla ya kusambazwa kwa watumiaji.
Pia, serikali imependekeza kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa usafirishaji wa mafuta, ambapo timu hiyo itahakikisha meli zote zinazoleta mafuta nchini zinatimiza ratiba yake na kushusha shehena bila kuelekezwa kwenye masoko mengine kwa sababu za kibiashara.
Waziri huyo amesisitiza kuwa taifa haliwezi kuvumilia ucheleweshaji wa mafuta, akibainisha kuwa mikataba iliyopo lazima iheshimiwe na mafuta yote yaliyopangwa kuletwa nchini yafike kwa wakati. Ameonya kuwa kucheleweshwa kwa shehena yoyote kunaweza kuathiri usambazaji na kusababisha changamoto kwa wananchi.
Hatua hizi zinakuja wakati dunia ikikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa nishati kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, hali inayoongeza umuhimu wa Tanzania kuwa na mikakati madhubuti ya kuhakikisha usalama wa nishati.
















