Trump aongeza shinikizo kwa Iran, atishia hatua kali iwapo hakutakuwa na makubaliano
Kwa mara nyingine, Rais wa Marekani Donald Trump ameibuka na mkakati wa shinikizo kali dhidi ya Iran kwa kutoa muda wa saa 48 kufikiwa kwa makubaliano, akionya kuwa Iran itakiona cha mtema kuni iwapo haitatii sharti hilo.
Katika hotuba yake kwa taifa tarehe 1 Aprili 2026, Rais Donald Trump alisisitiza kuwa operesheni ya kijeshi inaelekea kukamilika, akisema: “Tutamaliza kazi, na tutaimaliza haraka sana.”
Aidha, aliongeza kuwa mafanikio ya kijeshi tayari yanaonekana: “Tunapiga hatua kubwa kuelekea kukamilisha malengo yetu ya kijeshi.”
Hata hivyo, pamoja na kauli hizo za matumaini, Trump ameendelea kutoa vitisho vipya. Katika ujumbe wake wa hivi karibuni tarehe 5 Aprili 2026 kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz, aliitaka Iran kufungua njia hiyo muhimu ya mafuta, akionya kuwa vinginevyo Marekani itachukua hatua kali za kijeshi, ikiwa ni pamoja na kushambulia miundombinu muhimu kama vituo vya umeme na madaraja.
Hii si mara ya kwanza kutumia mbinu ya kutoa muda mfupi akifuatisha na vitisho vya nguvu ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na kauli zake za awali za kuirudisha Iran “katika zama za mawe."
Aidha, Trump aliiambia shirika la habari la Axios kwamba Marekani iko "katika mazungumzo ya kina" na makubaliano yanaweza kufikiwa.
"Kuna nafasi nzuri, lakini ikiwa hawatafanya makubaliano, nitalipua kila kitu huko," alisema.
Kwa upande wa Iran, msimamo wake hadi sasa uko pale pale, imeeleza kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz haijafungwa kabisa bali umefungwa kwa nchi inazoziona kama maadui.
Halikadhalika Iran imekataa kusitisha mapigano kwa muda, ikitaka uhakika wa kudumu wa kutoshambuliwa tena pamoja na fidia ya hasara iliyosababishwa na mashambulizi ya Marekani na Israel.
Pia imesema itazitoza meli zinazopita katika Mlango Bahari wa Hormuz kama njia ya kujifidia, hatua inayogeuza njia hiyo muhimu ya mafuta kuwa kitega uchumi.
Iwapo muda huo utaisha bila makubaliano, Trump ametishia kuivamia Iran na hata kuchukua udhibiti wa mafuta ya nchi hiyo. Hapo awali pia ametishia kutuma vikosi vya ardhini Iran, jambo ambalo wachambuzi wa kisiasa wamelieleza kuwa na uwezekano mdogo kutokana na hasara waliopata Marekani baada ya kuivamia Iraq na Afghanistan.
Wakati huo huo, gharama za vita zinaongezeka ambapo Trump tayari ametaka kuongezewa bajeti ili kuendeleza operesheni hizo.
Bei za mafuta zinaendelea kupanda, zikiziathiri zaidi nchi zinazoendelea hasa barani Afrika ambako dalili za uhaba tayari zimeanza kuonekana.
Ndani ya Marekani, Trump anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wananchi wanaotaka vita visitishwe kutokana na athari yake ya kiuchumi, lakini kutoka nje pia, hasa kutoka kwa nchi washirika, Trump anakabiliwa na shinikizo kama hilo, jambo linaloongeza uzito wa kisiasa katika mgogoro huu.