Moto wateketeza kambi ya wakimbizi Sudan Kaskazini mwa Darfur, wawili wafariki dunia
Moto huo ulikumba makazi ya muda huko Tawila huku msongamano wa watu na uhaba wa misaada ukizidisha mzozo wa kibinadamu wa Sudan.
Moto mkubwa umetokea katika kambi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao (IDPs) katika eneo la Tawila, jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, na kusababisha vifo vya watu wawili.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, moto huo ulizuka siku ya Jumatatu na kuenea kwa kasi katika makazi ya muda yaliyoko eneo la Hilla Naima mjini Tawila, takriban kilomita 60 magharibi mwa mji wa Al Fasher. Moto huo uliharibu nyumba kadhaa zilizojengwa kwa vifaa vya kienyeji na kuwaacha familia nyingi bila makazi.
Miongoni mwa waliofariki dunia ni mtoto wa miaka 12, amesema Yahya Ibrahim, mmoja wa wanachama wa Kamati ya Kutoa Huduma za Dharura katika mji wa Tawila.
Mji wa Tawila umekuwa kimbilio muhimu kwa raia wanaokimbia machafuko katika mji wa Al Fasher na maeneo ya jirani, hasa baada ya kikosi cha wanamgambo cha RSF kuuteka mji huo tarehe 26 Oktoba 2024.
Maelfu wameathirika
Kwa sasa, mji wa Tawila inahifadhi takriban watu 655,000 waliokimbia makazi yao, wengi wao wakitoroka Al Fasher kupitia njia hatarishi wakitafuta usalama.
Hapo awali, mamlaka za Sudan na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kikanda yameishtumu RSF pamoja na mshirika wao, kundi la ‘Sudan People’s Liberation Movement–North’, kwa kufanya ukiukwaji wa haki dhidi ya raia.
Mapigano yamezidi kushika kasi katika wiki za hivi karibuni katika majimbo matatu ya Kordofan — Kaskazini, Magharibi na Kusini — hali iliyosababisha makumi ya maelfu ya raia kuyahama makazi yao.
Kati ya majimbo 18 ya Sudan, RSF inadhibiti majimbo yote matano ya eneo la Darfur Magharibi, isipokuwa sehemu za Darfur Kaskazini ambazo bado ziko chini ya udhibiti wa jeshi la taifa.
Jeshi la Sudan linadhibiti maeneo mengi ya majimbo 13 yaliyosalia kusini, kaskazini, mashariki na katikati mwa nchi, ikiwemo mji mkuu, Khartoum.
Mgogoro kati ya jeshi la Sudan na RSF, ulioanza Aprili 2023, umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwafanya mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.