Pacquiao na Mayweather wakubaliana kuzipiga tena ulingoni

Floyd Mayweather na Manny Pacquiao watakabiliana tena katika pambano la ndondi linalotarajiwa kufanyika Las Vegas

By
Bondia Floyd Mayweather. / Reuters

Wakali wa masumbwi Manny Pacquiao na Floyd Mayweather wamekubaliana kupambana tena ulingoni mwezi Septemba.

Pacquiao, 47, na Mayweather, 48, watapigana Sphere huko Las Vegas siku ya Jumamosi, 19 Septemba.

Bingwa wa zamani wa dunia Mayweather ametangaza kuwa licha ya kustaafu anarudi tena kwa mara ya nne.

Itakuwa pambano la kwanza la kulipwa kwa Mayweather tangu alipompiga Conor McGregor 2017 katika raundi ya 10.

Raia wa Filipino Pacquiao alistaafu kutoka kwenye ndondi 2021 ili aangazie masuala ya siasa alirudi tena ulingoni Julai mwaka jana na kupigana na bingwa wa welter wa WBC Mario Barrios, ambaye alibaki na ubingwa wake baada ya pambano hilo kumalizika kwa sare.

Mayweather na Pacquiao walipambana kwa mara ya kwanza 2015, kwa kile kilichofahamika kuwa 'Pigano la Karne' na bado limebaki kuwa lilohusisha fedha nyingi zaidi katika historia ya masumbwi.

Mayweather ndiye aliyeibuka mshindi kwenye ngumi hizi, akimshinda Pacquiao kwa wingi wa alama huko Las Vegas.

Haifahamiki pambano hilo litakuwa la raundi ngapi na ni uzani gani utakaopiganiwa.