| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mahakama Marekani yatoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa zamani wa Cuba Raul Castro
Rais huyo wa zamani wa Cuba anatuhumiwa kwa kupanga njama ya kuwaua watu 4 waliokuwa kwenye ndege 2 za kiraia, huku nyaraka za mahakamani zikidai kuwa majasusi wa Cuba walitoa taarifa za safari kabla ya ajali ya ndege kutokea
Mahakama Marekani yatoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa zamani wa Cuba Raul Castro
Rais Mstaafu wa Cuba Raul Castro

Jaji wa Mahakama ya Miami ametoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa zamani wa Cuba mwenye umri wa miaka 95, Raul Castro kuhusiana na ajali ya ndege mbili za kiraia iliosababisha vifo vya watu wanne, ikiwemo raia watatu wa Marekani 1996.

Hati hiyo inamtuhumu Castro kwa kupanga njama na maafisa wa ujasusi wa Cuba kuua. Ilitiwa saini siku ya Ijumaa kufuatia uchunguzi wa Idara ya Usalama ya Jimbo la Florida, kulingana na nyaraka za mahakamani zilizoonekana na Miami Herald na Tampa Bay Times.

Zinaonesha kuwa Florida ina uwezo wa kumshtaki Castro kwa sababu zinadai kuwa majasusi wa Cuba “walijipenyeza” ndani ya kundi la Brothers to the Rescue maeneo ya Miami na Key West na kutoa taarifa kwa mamlaka za Cuba kabla ajali hiyo kutokea.

Kundi la Brothers to the Rescue lina makao yake Florida na ni shirika lisilo la Kiserikali lililoundwa na raia wa Cuba walio uhamishoni ambao wanafahamika kupinga serikali ya Cuba.

Kulingana na taarifa, majasusi hao wa Cuba waliwaarifu watu wao wasisafiri na kundi hilo kati ya Februari 24-27, 1996. Mmoja ya watu hao aliondoka Florida na kurudi Cuba Februari 23, siku moja kabla ya ndege hizo kudunguliwa.

Februari 24, 1996, ndege za kivita za Cuba zilidunguwa ndege mbili ndogo zinazosimamimwa na kundi la Brothers to the Rescue, na kusababisha vifo vya watu wanne waliokuwemo ndani.

Cuba inadai kuwa ndege hizo zilikuwa kwenye anga yake na kutetea uamuzi huo kama hatua ya kujilinda, ilhali Marekani inasema ilikuwa katika maeneo ya kimataifa.

Castro, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa majeshi, pia alishtakiwa na Wizara ya Haki ya Marekani mwezi Mei kwa mauaji na kupanga njama ya kuua.

Hati hii ya kukamatwa kutoka jimbo la Florida ni hatua nyingine katika kesi ambayo kwa miongo kadhaa kumetolewa wito wa mashtaka, huku miaka 30 tangu kutokea kwa ajali hiyo ikikumbukwa mwaka huu.

Raul Castro ni kaka yake marehemu Fidel Castro, ambaye aliliongoza taifa hilo la kisiwa kwa karibu miaka 50 na kufariki 2016. Alikuwa rais wa Cuba kuanzia 2008 hadi 2018, akimrithi Fidel, ambaye alimkabidhi madaraka kwa muda mwaka 2006 wakati alipokuwa mgonjwa.

CHANZO:َAA