Rais wa Uganda Museveni amewezaje kuwepo madarakani kwa miaka 40?
Rais Yoweri Museveni ameeleza kuwepo kwake madarakani kwa muda mrefu ni kutokana na ulazima wa mazingira na wala siyo maslahi binafsi ingawa wachanganuzi wanasema ni kutokana na kuwa katika eneo la kimkakati.
Kwa raia wengi wa Uganda, Yoweri Museveni ndiye rais pekee wanaemfahamu hasa baada ya kushinda muhula wake wa saba katika uchaguzi uliokamilika.
Alishinda kwa asilimia 71.65 ya kura, Tume ya Uchaguzi ilisema, na chama chake kinachotawala, National Resistance Movement (NRM) kinatarajiwa kuwa na wabunge wengi zaidi bungeni. Upinzani wametaja matokeo hayo “kuchakachuliwa”.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 — aliyeingia madarakani 1986 baada ya vita vya msituni – ni miongoni mwa viongozi wenye umri mkubwa walio madarakani na mkuu wa nchi wa tatu kuwepo madarakani kwa muda mrefu barani Afrika.
Wanaomuunga mkono wanaona kipindi chake cha miaka 40 kama kimekuwa na tija katika kuhakikisha usalama wa nchi wakati ambapo mataifa jirani yamekuwa yakikabiliwa na misukosuko. Uganda imewahi kukabiliwa na mapinduzi tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza 1962 - huku viongozi tisa wakiondolewa madarakani katika kipindi cha zaidi ya miaka 22 - hadi pale Museveni aliposhika hatamu.
Mafanikio
Katika kutafuta muhula wake wa saba, kiongozi huyo aliikita kampeni yake kwa ahadi za kuipeleka nchi katika uchumi wa kati. Nchi hiyo inaelekea kuanza kuuza mafuta huku kampuni ya mafuta ya Ufaransa TotalEnergies na ile ya umma ya China,CNOOC ikitarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Oktoba.
Wachanganuzi wanasema kuwa kuwepo kwa Museveni kwa muda mrefu kunatokana na yeye kuwa eneo la kimkakati katika jukwaa la kimataifa na kuwa na vikosi vyake kila mahali katika nchi.
Amechangia vikosi katika operesheni za kulinda amani katika kanda na amepongezwa kwa kuwa na makazi makubwa duniani ya wakimbizi.
“Anakubalika na mataifa ya Magharibi kwa sababu anashughulikia maslahi yao katika kanda hiyo,” Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Uganda Kiiza Eron ameiambia TRT Afrika.
“Na hata wakati kuna usalama, ni usalama unaotegemea mtu mmoja.”
Kuna wasiwasi kuhusu uhuru wa taasisi za umma na jukumu la familia yake katika serikali. Mke wa Museveni ni waziri wa elimu katika baraza lake la sasa la mawaziri, mtoto wake wa kiume Jenerali Muhoozi Kainerugaba ni mkuu wa majeshi, huku kaka yake wa kambo Salim Saleh akiwa mshauri wa rais wa masuala ya kijeshi.
Ukosefu wa ajira kwa vijana na kuonekana kama wametengwa katika siasa za nchi hiyi ilikuwa miongoni mwa malalamiko makuu kwenye uchaguzi.
"Nimekuwa nikimuona yeye (kama rais) tangu nilipozaliwa. Amekuwa madarakani kwa kipindi hicho kirefu kutokana na mbinu zake," Sultan Ahmed Ikonge ameiambia TRT Afrika.
Kumekuwa na mjadala kuhusu nini kitafanyika baada ya Museveni kutokuwepo madarakani. Lakini wachanganuzi wanasema tayari mpango wa kumrithi umeandaliwa, huku mtoto wake mwenye umri wa miaka 51 akionekana kuwa na ushawishi ikiwa ishara kuwa ndiye anayeandaliwa kuchukua mikoba.
"Tayari ameandaa mpango wa kumrithi. Wamekuwa wakilifanyia kazi hili kwa muda mrefu … Kwa hiyo ilivyo sasa, mpango wa kumrithi umefikia hatua ya nusu na wataendelea kuufanyia kazi,” anasema Eron.