| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Ghana yasema imetumia $4.37 milioni kuwarudisha raia wake nyumbani kutoka Afrika Kusini
Waziri anasema hali hiyo haikuwa imetarajiwa kwa hiyo haikuwa imekadiriwa kwenye bajeti ya serikali.
Ghana yasema imetumia $4.37 milioni kuwarudisha raia wake nyumbani kutoka Afrika Kusini
Ablakwa anasema serikali ilianza kuwarudisha nyumbani raia wake baada ya hali ya usalama kuzorota katika baadhi ya maeneo Afrika Kusini.

Ghana imetumia karibu $4.37 milioni kuwasafirisha raia wake 1,964 kutoka Afrika Kusini kufuatia "mashambulizi ya chuki na vitisho dhidi ya raia wa kigeni," serikali imesema.

Waziri wa Mambo ya Nje Samuel Okudzeto Ablakwa amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa safari hizo zilizoanza Mei 27 hadi Septemba 4, 2026, zimegharimu GH¢49.72 milioni ($4.37 milioni).

Shirika la habari la Ghana limeripoti kuwa shughuli hizo zilijumuisha ndege za kukodisha na za kawaida, kuwapeleka watu hadi makwao, malazi, chakula na matibabu kwa ajili ya waliokuwa wanarudi nyumbani.

Ablakwa anaeleza mchanganuo huo kuwa GH¢38.84 milioni ($3.41 milioni) zilitumika kwa ajili ya ndege, tiketi, kuwasafirisha watu, chakula, hoteli nchini Afrika Kusini, matibabu na kulazwa hospitali.

Nyingine GH¢10.80 milioni ($949,677) zilitumika katika kuwajumuisha watu katika jamii na posho ya usafiri, ilhali GH¢84,274 ($7,409) zilikuwa kwa ajili ya kurudisha miili ya raia wawili nyumbani.

Ablakwa anasema kila kitu kimelipiwa kamili, na kwamba hakuna deni.

Kila aliyerudi nyumbani alipewa GH¢5,000 ($440) kama fedha za kuanza maisha na GH¢500 ($44) gharama za usafiri.

Pia walifanyiwa vipimo vya matibabu bila malipo, kusajiliwa katika Mpango wa Bima ya Afya ya nchini Ghana, vyakula na kadi za simu walizowekewa data na vocha.

CHANZO:TRT Afrika Swahili