Ujerumani yatoa wito wa kuunda “ushirikiano wa kimkakati” ili kukabiliana na changamoto za kimataifa

Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, ametoa wito wa kuunda “ushirikiano wa kimkakati” ili kukabiliana na changamoto za kimataifa wakati wa ziara yake mjini Ankara.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz katika mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji, Oktoba 23, 2025. /

Friedrich Merz amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu zaidi katika masuala ya sera za kigeni, usalama, nishati na biashara, kabla ya kukutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

“Uturuki na Ujerumani zinashirikiana kwa namna ya kipekee na ya kina — katika sera za kigeni na usalama, pamoja na masuala ya uhamiaji, nishati na biashara,” Merz aliandika kwenye chapisho la mitandao ya kijamii kabla ya mkutano wake na Erdogan siku ya Alhamisi.

Kiongozi huyo wa Ujerumani pia alisisitiza dhamira yake ya kukuza “ushirikiano wa kimkakati” ili kukabiliana na changamoto mpya za kijiografia duniani.

“Tunaingia katika awamu mpya ya kijiografia. Hivyo, tunapaswa kupanua ushirikiano wetu wa kimkakati,” alisema, akiongeza kuwa, “Nataka kuimarisha zaidi ushirikiano wetu wa karibu. Ndiyo maana niko Ankara kukutana na Recep Tayyip Erdogan.”

Kansela Merz, ambaye aliiunda serikali mpya ya muungano wa Ujerumani mwezi Mei, amefannya ziara yake ya kwanza rasmi mjini Ankara siku ya Alhamisi.

Masuala ya Ukraine na ulinzi kwenye ajenda

Ziara hiyo inatarajiwa kujikita zaidi kwenye vita vinayoendelea nchini Ukraine na juhudi za kuleta amani Mashariki ya Kati, ambako Uturuki imejitokeza kuwa mpatanishi muhimu.

Mazungumzo hayo pia yanatarajiwa kugusa mada nyingine kuu kama uhamiaji na ushirikiano wa kijeshi.

 Maendeleo makubwa katika sekta ya ulinzi yalishuhudiwa mapema wiki hii, baada ya kutiwa saini makubaliano siku ya Jumatatu kuhusu usambazaji wa ndege za kivita aina ya Eurofighter kwa Uturuki.

Ndege hizo huzalishwa Uingereza chini ya mpango wa pamoja unaojumuisha Ujerumani, Italia na Hispania — na unahitaji idhini ya mataifa yote manne kabla ya mauzo yoyote kufanyika.

Serikali ya Ujerumani imeelezea ziara hiyo kuwa ya muhimu, huku msemaji wake akisema ni fursa ya kuimarisha mazungumzo na ushirikiano kuhusu masuala makubwa ya kimataifa na ya kikanda.

“Uturuki ina nafasi muhimu — si tu kama mshirika wa NATO bali pia kama mshirika wa mazungumzo katika masuala mengi ya kisiasa ya kimataifa,” alisema Naibu Msemaji wa Serikali, Steffen Meyer, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin.

SOURCE: TRT World & Agencies