Watu 30 wamepoteza maisha kufuatia mvua kubwa zilizolikumba eneo la Gamo, kusini mwa Ethiopia, serikali ya nchi hiyo imesema.
"Tunasikitika kutangaza vifo vya watu 30 kutokana na mvua kubwa iliyoshuhudiwa hususani katika maeneo ya Degama,” ilisema idara ya mawasiliano ya Gamo, kupitia taarifa yake kwenye mtandao wa Facebook siku ya Jumanne.
Hali kama hiyo imeshuhudiwa katika mataifa mengine katika ukanda wa Afrika Mashariki katika siku za hivi karibuni.
Mwishoni wa juma lililopita, watu 43 waliripotiwa kupoteza maisha nchini Kenya, huku wengine 50,000 wakiachwa bila ya makazi kufuatia mvua kubwa zilizoshuhudiwa nchini humo.
Barabara nyingi za jiji la Nairobi, ziligeuka kuwa mito, shughuli za usafiri zikikwama siku ya Ijumaa haswa katika barabara kuu ya Nairobi – Mombasa.
















