Usafiri wa anga Mashariki ya Kati waendelea kuathirika
Kulingana na kampuni ya uchanganuzi wa safari za anga ya Cirium, zaidi ya abiria milioni moja wameathiriwa na zaidi ya safari za ndege 19,000 kati ya 51,600 zilizopangwa kuingia na kutoka Mashariki ya Kati zimesitishwa tangu kuanza kwa mashambulizi
Maelfu ya abiria bado wamekwama huku safari za ndege za kibiashara katika maeneo ya Mashariki ya Kati zikiwa zimekwama.
Usafirishaji wa mizigo nao pia umekwama.
Hii ni baada ya usafiri wa anga katika eneo la Mashariki ya Kati kuendelea kusitishwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, huku Iran ikilipiza.
Kulingana na kampuni ya uchanganuzi wa safari za anga ya Cirium, zaidi ya abiria milioni moja wameathiriwa na zaidi ya safari za ndege 19,000 kati ya 51,600 zilizopangwa kuingia na kutoka Mashariki ya Kati zimesitishwa tangu kuanza kwa mashambulizi Februari 28.
Nchi za Afrika zikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda zimetoa ushauri wa usafiri na usalama kwa raia wake wanaoishi au wanaopitia mataifa ya Ghuba, bila mipango ya haraka ya kuwahamisha.
Ndege za abiria na mizigo zilizopangwa kuondoka kuelekea Mashariki ya Kati ziliendelea kuegeshwa katika viwanja vya ndege.
Wasafirishaji wakubwa zaidi wa Mashariki ya Kati wameondoa uwezekano wa kuanza tena safari za ndege zilizopangwa hadi angalau Machi 5, 2026 wakati mzozo wa Marekani na Israeli dhidi ya Iran ukiendelea, na hivyo kudhoofisha matumaini ya kurejea haraka kwa safari za kawaida za anga.
Wasafiri wengi waliokwama walianza kuhamishwa na nchi zao kutoka UAE kwa idadi ndogo siku ya Jumatatu, huku serikali duniani kote zikijitahidi kuwaondoa raia wao kutoka eneo hilo.
India na Uhispania kwa mfano zimeanza kuhamisha raia wake huku nchi nyengine zikifanya utaratibu.
Kampuni ya Etihad, yenye makao yake makuu Abu Dhabi, ilisema huduma zake za kibiashara zilisitishwa hadi Alhamisi Machi 5, huku Emirates ikisema ikikataza safari za ndege zilizopangwa hadi saa sita usiku Jumatano 4th March.
Qatar Airways ilisema itatoa sasisho zaidi Jumatano lakini anga yake ilibaki imefungwa kwa safari zote za ndege.
Mashirika ya ndege ya Etihad na Emirates, pamoja na shirika la usafiri wa bei nafuu la FlyDubai, yalisema yataendelea na safari chache tu za mizigo na kurudisha watu makwao.
Hali hii inaweza kuendelea kwa wiki kadhaa, hii ni baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba mzozo huo ulitarajiwa kuendelea kwa wiki nne hadi tano, lakini unaweza kuwa chini ya hapo.
Kwa mashirika ya ndege ya kibiashara, mzozo huo uliibua kumbukumbu za majanga kama yale ya ndege ya Malaysia MH17, iliyoharibiwa na kombora kuelekea Ukraine mnamo 2014 ambapo watu 298 waliuawa.
Pia kulikiwa na kisa cha ndege ya Boeing ya Ukraine iliyodunguliwa kwa bahati mbaya na Iran mnamo 2020, na kuua 176.
Kwa hiyo, kinachofanyika sasa hivi ni tahadhari ya kuepusha majanga kama hayo.
Changamoto ni kwa waliokwama ambao mpaka sasa hawajajua lini watarudi makwao.
Wafanyabiashara nao waliotegemea bidhaa kupitia angani au kusafiri kwenda kununua bidhaa wako katika hali ya mfadhaiko, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya Sikukuu ambapo ni msimu wa wafanyabiashara kuvuna.
Kwa mara nyengine, sekta ya usafiri wa anga duniani inajipata katika hali tete, hata kabla haijajikwamua kutokana na hasara ya janga la Uviko 19.