Afrika yajivunia mafanikio makubwa 2025

Kuanzia teknolojia, ubunifu, sanaa na uvumbuzi, mwaka wa 2025 umeona Waafrika wakijiunga kwenye mbio za kutafuta ushindi sio kuinua tu majina yao bali nchi za na hata bara kwa ujumla.

By Yusuf Dayo
Miongoni mwa zawadi kubwa Afrika inatoa kwa ulimwengu ni wanamichezo. Na mwaka huu bara lilijikakamua kuonyesha vipaji./ CAF / CAF

Kama kuna kitu cha kusisimua kwa wananchi ni kusikia wenzao wametajwa katika nyanja za kimataifa.

Kenya ilikaribia kupata rekodi ya kimataifa ya Guiness, pale msichana Truphena Muthoni alipokumbatia mti kwa zaidi ya saa 72. Japo bado Guiness haijathibitisha rekodi hiyo, Wakenya walijitokeza kwa maelfu kumtia moyo na hata kujaribu kushinikiza Guiness kumtambua binti huyo.

Lakini sasa msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 amepokewa kwa shangwe na Rais wa Kenya ambaye amemteua kama balozi wake wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira.

Lakini hii ina maana kuwa Waafrika wamekuwa na hamu kubwa ya matukio ya kusherehekewa ili kuonesha na wao pia wana vipaji na pia kupumua kutokana na masaibu ya mwaka mzima.

Mfano, kuna nchi kama Nigeria ambayo mwaka huu pekee imeingia kwenye kumbu kumbu kwa kuvunja rekodi tatu za dunia za Guiness.

Wanigeria wawemeka rekodi ya Mkusanyiko mkubwa zaidi wa walimu (20 Septemba), mbunifu wa Nigeria Kuforiji Oluwaseun alikamilisha ushonaji wa saa 106 kwa kutumia sindano na uzi, na kijana mwenye umri wa miaka 15, Kanyeyachukwu Tagbo-Okeke, alitengeza turubai kubwa zaidi katika historia ya dunia.

Tanzania pia waliweka rekodi ya upigaji ngoma wa muda mrefu zaidi duniani na kusifiwa kwa kuonesha ustahamilivu wa tamaduni.

Ukuaji wa Teknolojia na misheni za sayari ya mbali

Mbio za kukimbilia sayansi ya utafiti wa anga za mbali zilishika kasi mwaka 2025.

Takriban nchi 6 za Afrika zilizindua moja kwa moja mpango wa setilaiti za uangalizi wa dunia kuanza 2025.

Djibouti - Ilizindua mradi wake wa kwanza wa Uchunguzi wa Dunia Aprili 2025 kwa usaidizi wa Ufaransa - hatua ya kihistoria kwa sekta ya anga ya juu nchini.

Botswana- Ilizindua BotSat-1 Machi 2025, na kuongeza kwenye kundi linalokua na setilaiti barani Afrika zinazotumika kwa uchunguzi wa dunia na utumiaji wa data kama vile kwenye kilimo, ufuatiliaji wa hali ya hewa na ufuatiliaji wa majanga.

Nigeria - Ilitangaza idhini ya kuzindua setilaiti nne mpya mwaka wa 2025, ikiwa ni pamoja na setilaiti tatu maalum za uchunguzi wa dunia na setilaiti moja ya sintetiki-aperture rada (SAR) - Synthetic Aperture Rada (SAR), aina ya rada ambayo inachukua picha za kina za dunia kwa kutumia mawimbi ya redio badala ya mwanga. Kwa sababu haitegemei mwanga wa jua, SAR inaweza: kuona mchana na usiku na kutazama kupitia mawingu, moshi, na mvua nyepesi.

Misri - Kuendelea kwa matumizi amilifu na uzalishaji wa taarifa kutoka MisrSat-2, setilaiti ya Misri ya uchunguzi wa dunia ambayo tayari inafanya kazi mwaka wa 2025. Misri pia iliandaa uzinduzi wa Shirika la Anga la Afrika (AfSA) mwezi Aprili 2025, kusaidia zaidi uratibu wa uchunguzi wa Dunia kote barani.

Afrika yasalia kidedea michezoni

Miongoni mwa zawadi kubwa Afrika imetoa kwa ulimwengu ni katika sekta ya michezo. Na mwaka huu bara lilijikakamua kuonesha vipaji. Afrika Mashariki ilikuja pamoja katika kuandaa shindano kubwa la CHAN lililoishia kwa ufanisi mkubwa. Kombe lilikwenda Morocco lakini kwa Kenya, Tanzania na Uganda, ilikuwa kujipima uwezo wake katika maandalizi ya kombe la taifa bingwa mwaka 2027 ambayo pia wataandaa kwa pamoja.

Mashindano ya Riadha ya Dunia ya 2025 yalijumuisha maonesho bora ya Kiafrika kama vile: Kenya ikipata medali nyingi za dhahabu na maonesho bora katika mbio za mita 800, kuruka viunzi na marathoni.

Timu ya Botswana ya mbio za kupokezana vijiti 4x400m ilishinda dhahabu ya kihistoria - ya kwanza kwa Afrika katika mashindano hayo ulimwenguni.

Medali kadhaa za kibinafsi kutoka kwa wanariadha kote Nigeria, Ethiopia na Tanzania, zinaonesha uwepo mkubwa wa bara kwenye jukwaa la dunia.

Katika shindano kubwa la ‘Adizero Road to Records’ mnamo Aprili 2025, mwanariadha Mkenya Agnes Ngetich alikuwa mwanamke wa kwanza kuvunja rekodi ya chini ya dakika 30 kwa wanawake pekee, akitumia saa 29:27 - rekodi mpya ya ulimwengu ya kilomita 10 pekee ya wanawake. Rekodi hii ilikubaliwa rasmi na shirika la Riadha duniani.

Wanariadha mashuhuri kama Faith Kipyegon na Bouchra Hajij walitajwa kuwa miongoni mwa watu walio na ushawishi mkubwa katika michezo barani Afrika mnamo 2025.

Hatua kubwa kuimarisha afya Afrika

Huku utafiti ukisemekana kushika kasi katika sekta ya afya barani Afrika, ambapo kumekuwa na majaribio kadhaa ya tiba na chanjo. Mojawapo ya changamoto kubwa ya maambukizi barani imekuwa virusi vya Ukimwi VVU.

Msukumo kuwa ugonjwa huo umeathiri Afrika zaidi ulimwenguni, ni wajibu kuwa bara limehusika katika utafiti wa chanjo dhidi yake.

Kwa mara ya kwanza kwa chanjo ya kuzuia maambukizi imeanza kutumika katika mataifa ya Afrika Kusini, Eswatini na Zambia mnamo Jumatatu, Disemba 1.

Mbali na hilo, wataalamu wa afya barani Afrika, wameonesha ustadi na ukuaji mkubwa kitaaluma huku wakifanikisha upasuaji wa aina mpya mbali mbali kwa mara ya kwanza.

Mfano Afrika Kusini iliweza kufanya upasuaji wa kwanza kutumia Akili Bandia na roboti moja kwa moja huku mpasuaji akiwa nchini Marekani. Nigeria madaktari walifanya upasuaji wa kwanza wa wazi wa moyo.

Morocco walifanya upasuaji wa kwanza wa kupandikiza figo ambapo mchangiaji na mpokeaji hawakuwa na damu aina moja.

Nchini Kenya madaktari walifanikisha ufufuaji wa mfumo wa neva kwa sehemu ya mguu uliokatwa.

Haya yote yanaweka imani chanya kwa maendeleo ya kimatibabu barani Afrika miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yanayotajika Kimataifa.

Na mwaka ujao 2026, malengo makubwa zaidi yamewekwa na nguvu zaidi katika ufanikishaji.