Maelfu waondoka katika makazi yao Sudan Kusini kutokana na mapigano

Majeshi hasimu yanakabiliana katika ngome ya upinzani mji wa Akobo nchini Sudan Kusini, vyanzi vilisema siku ya Jumatano, kufanya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

By
Hali ya taharuki Sudan Kusini baada ya mapigano kati ya jeshi na vikosi vya upinzani kuongezeka. / Reuters

Majeshi hasimu yamekabiliana katika ngome ya upinzani mji wa Akobo, Sudan Kusini, vyanzo vilisema siku ya Jumatano, kufanya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Akobo uko katika jimbo la mashariki la Jonglei na ni sehemu ya hivi karibuni kuwa na makabiliano makali kati ya serikali na vikosi vya upinzani.

Siku ya Ijumaa, jeshi liliagiza mashirika ya misaada ya kigeni kuondoka katika mji huo likijiandaa kufanya mashambulizi ili kurudisha udhibiti wa serikali.

Huku kukiwa na mapigano, upinzani unasema bado unadhibiti makao makuu ya eneo hilo, ukikanusha taarifa za awali kuwa jeshi limemrudisha kamishna "halali" wa eneo hilo.

Watu wengi wameondoka katika makazi yao

Chanzo kimoja kutoka kwa taasisi ya usalama nchini Sudan Kusini kimeiambia AFP kuwa jeshi liliingia Akobo siku ya Jumanne, na kumekuwa na mapigano kote katika mji.

Watu karibu 200,000 wameondoka katika makazi yao hadi katika eneo la karibu la Tiergol kwenye mpaka wa Ethiopia, chanzo hicho kilisema.

Huku kukiwa hakuna mawasiliano ya kutosha, imekuwa vigumu kuthibitisha yanayoendelea katika eneo hilo.

Umoja wa Mataifa umekataa kuondoka kutoka Akobo, lakini mashirika mengine yasiokuwa ya serikali kama Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) yamelazimika kuondoka siku ya Jumamosi.

Uhasama wa Kiir, Machar

Sudan Kusini ilipata uhuru 2011 lakini muda mfupi baadaye ikaanza vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Rais Salva Kiir kutofautiana na makamu wake, Riek Machar.

Makubaliano ya kugawana madaraka ya 2018 kati ya Rais Kiir na Machar yamekuwa yakisuwasuwa tangu mapema 2025, huku kukiwa na mapigano katika maeneo mbalimbali.