Kituo Kikuu cha Afya barani Afrika kimesema siku ya Alhamisi kuwa kinalenga kuwa na chanjo na tiba ya maambukizi ya Bundibugyo yatokanayo na Ebola kufikia mwishoni mwa mwaka huu, huku wahudumu wa afya wakipambana kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo unaoenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi jirani ya Uganda.
“Tunachoweza kukuambia kwa uhakika-kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2026-kituo cha afya cha Afrika CDC kitahakikisha kwamba tuna chanjo na tiba dhidi ya Bundibugyo,” amesema Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa.
Kwa upande wake, Shirika la Afya Duniani WHO, limesema utafiti wa chanjo na matibabu ya Bundibugyo, sharti ufanyike kwa ajili ya utafiti huku wataalamu wakitathmini usalama wao na ufanisi wa tiba.
Mpaka sasa, hakuna chanjo iliyothibitishwa inayolenga kutibu kirusi cha Bundibugyo, imesema WHO, ingawa watu kadhaa wametengwa kwa ajili ya majaribio.
WHO imesema inashirikiana na Congo na Uganda, pamoja na washirika wengine ikiwemo kituo cha Afya cha Afrika CDC, kujaribu kufanya majaribio kwa kufuata ipasavyo misingi na viwango vinavyohitajika.
Mlipuko, ulioenea zaidi mashariki kwa Congo, tayari umesababisha maambukizi ya watu 900 na vifo vinavyoshukiwa 220, hii ni kwa mujibu wa takwimu za WHO.
Uganda kwa upande wake, imethibitisha kuwepo kwa maambukizi kadhaa.
Wahudumu wa afya wanapamba kuwafuatilia maelfu ya watu wanaoshukiwa kuwa na maambukizi, lakini jitihada hizo zinaathiriwa na mgogoro unaoendelea, vituo vya afya kushambuliwa, upungufu wa vifaa tiba na kuenea kwa hali ya kutoaminiana katika jamii iliyoathirika.



















