Mataifa wanachama ya Shirika la Afya Duniani yanakutana kwa kongamano la kila mwaka jijini Geneva siku ya Jumatatu huku kukiwa na wasiwasi kuhusu milipuko ya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo na hofu ya Marekani na Argentina kutangaza kujiondoa.
Suala la mlipuko wa virusi vya hanta ambavyo vilipatikana katika meli ya kifahari halijaweka katika agenda rasmi, linatarajiwa kujadiliwa, kama ilivyo kwa mlipuko mwingine wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Chanzo kimoja cha kidiplomasia, ambacho hakikutaka kutajwa, kimesema kuwa itakuwa muhimu kuona namna gani WHO itaangazia milipuko hiyo "kuimarisha masuala mengine", ikiwemo "kushinikiza (Marekani na Argentina) wasijitoe".
Mkutano huo wa maamuzi wa kila mwaka wa WHO, ambao unaendelea hadi Jumamosi, unakuja baada ya shirika hilo kupitia mwaka mgumu. Limedhoofishwa na Marekani kutangaza kujiondoa na kupunguza ufadhili jambo lililofanya wapunguze bajeti yao pamoja na wafanyakazi.
Kutafuta fedha
"Tuko sawa sasa hivi na tunaendelea vizuri," Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisisitiza mwishoni mwa mwezi Aprili.
Hali "bado ni tete, lakini wamekuwa wakitafuta fedha" zinazohitajika kwa ajili ya miaka miwili ijayo, Surie Moon, mkurugenzi mwenza wa Shirika la Afya lililoko katika Taasisi ya Geneva, ameiambia AFP.
Na tatizo na virusi vya hanta "ni ishara tosha ya kwa nini dunia inahitaji WHO yenye ufadhili thabiti, wa kuaminika, usio egemea upande wowote, na wa uhakika ‘‘, aliongeza.
Mkutano huo unafanyika huku mchakato wa uchaguzi wa mkuu mpya wa shirika hilo la WHO ukishika kasi.
Hakuna mtu yeyote aliyetangaza kugombea nafasi hiyo kufikia sasa, lakini inawezekana wagombea wakajitokeza wiki hii kabla ya muda wa mwisho wa kuwasilisha maombi Septemba 24.













