Aamron, msanii maarufu wa kufokafoka anayejulikana kwa kukosoa uongozi wa Rais Faure Gnassingbe, alionekana tena siku ya Alhamisi kwa njia ya video akiomba radhi baada ya kuzuiliwa na polisi kwa zaidi ya wiki moja, akisema anajuta kutoa matamshi ya "matusi" kuhusu kiongozi huyo wa nchi.
Aamron, ambaye jina lake halisi ni Essowe Tchalla, alikamatwa nyumbani kwake katika mji mkuu, Lome, 26 Mei, saa kadhaa baada ya kuhamasisha watu kumfanyia kejeli Rais Faure Gnassingbe 6 Juni ambayo ni siku ya kusherehekea kuzaliwa kwa rais, alisema mama yake kupitia mtandao wa kijamii.
Kukamatwa kwake kulisababisha hasira kutoka kwa makundi ya upinzani na mashirika ya kijamii, ambayo yalikashifu kile walichokiita kuwa ukandamizaji wa wakosoaji.
Gnassingbe amekuwa rais wa Togo tangu 2005, alipomrithi baba yake ambaye alitawala taifa hilo kwa karibu miongo minne. Hivi karibuni alijitengenezea madaraka zaidi kwa kubadilisha mfumo kuwa wa bunge na yeye mwenyewe akiwa mkuu wa bunge hilo.
'Kuomba radhi kwa dhati'
"Nimetengeneza video kadhaa ambazo nimemtukana na kutumia lugha chafu dhidi ya Rais wa Baraza, Faure Gnassingbe," Tchalla alisema kupitia video, ambayo ilisambazwa katika mitandao ya kijamii.
"Ningependa kuchukua fursa hii kuomba msamaha na kumuomba radhi Mheshimiwa Faure Gnassingbe."
Tchalla anasema alipelekwa katika kituo cha watu wenye matatizo ya akili eneo la Zebe, karibu kilomita 50 mashariki mwa mji wa Lome, kwa kile alichokieleza kuwa na "msongo wa mawazo."
"Baada ya matibabu ya siku kadhaa, leo nahisi nimetulia zaidi na nimegundua tatizo la matamshi yangu na makosa yangu," alisema.
'Kukamatwa kwa ajili ya kutibiwa'
Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi, msanii huyo alikamatwa ili "atibiwe."
"Hakuwa anajifahamu," afisa mmoja wa polisi aliliambia shirika la habari la AFP.
Lakini wanasiasa na jamaa zake Tchalla walikanusha madai hayo.
"Aamron alikamatwa kutokana na uanaharakati wake," alisema Nathaniel Olympio, msemaji wa kundi la ‘Don't Touch My Constitution Front’, muungano wa vyama vya upinzani na mashirika ya kijamii.
Mwanaharakati mwingine, Honore Sitsope Sokpor – anayejulikana mitandaoni kwa jina la "Affectio" – amefungwa jela tangu mwezi Januari kutokana na kuweka shairi kwenye mitandao ya kijamii.











