Mechi ya kirafiki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya Chile itachezwa bila mashabiki katika mji wa Ufaransa wa Orleans siku ya Jumanne, msemaji wa timu hiyo amethibitisha.
Mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa katika mji wa Cadiz Hispania, lakini meya wa jiji hilo akapiga marufuku mechi hiyo kutokana na wasiwasi kuhusu mlipuko wa virusi vya Ebola kwenye nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Timu hiyo inafanya mazoezi yake katika mji wa Hispania wa Marbella baada ya kukamilisha kambi ya mazoezi ya siku 10 nchini Ubelgiji, ambapo walitoka sare 0-0 na Denmark siku ya Jumatano.
Maafisa wa Marekani wamewaambia wachezaji kuwa walihitajika kuwa nje ya DRC kwa muda wa siku 21 na wasiwe na dalili za virusi kabla ya kuruhusiwa kucheza katika Kombe la Dunia.
Ureno, Colombia, Uzbekistan kupambana na DRC Kombe la Dunia
Wachezaji wote 26 wanacheza nje ya DRC na vilabu vya Ulaya, ilhali maafisa kadhaa wamesafiri kutoka nchini humo ili kuingia kabini. Wote wametimiza masharti, kulingana na maafisa wa timu.
Baada ya kutoka Hispania, timu ya Congo itasafiri katika kambi yao ya Kombe la Dunia huko Houston siku ya Alhamisi. Wanaanza mechi yao ya kundi K dhidi ya Ureno siku sita baadaye, kabla ya kukabiliana na Colombia huko Guadalajara Juni 23 na Uzbekistan jijini Atlanta Juni 27.
Kufikia Jumamosi, idadi ya maambukizi ya Ebola yaliyothibitishwa nchini humo iliongezeka hadi 488, ikiwemo vifo 86.

















