Mahakama ya Morocco yawatupa jela mashabiki 19 wa soka kwa vitendo vya kihuni
Mahakama ya Morocco imewahukumu mashabiki 19 wa soka kifungo cha mwaka mmoja jela kwa vitendo vya kihuni walivyovionesha wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal, ambapo walijaribu kuvamia uwanja.
Baada ya kikao cha mahakama kilichodumu kwa zaidi ya saa tano, Jaji aliyekuwa akiongoza kesi hiyo aliamua kuwa mashabiki hao — raia 18 wa Senegal na mmoja wa Ufaransa — walikuwa na hatia ya zaidi ya mashtaka sita, yakiwemo kuharibu miundombinu ya michezo na kufanya vurugu wakati wa tukio la michezo.
Watu 11 walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutozwa faini ya dola 550. Wanne walihukumiwa kifungo cha miezi sita na faini ya dola 218. Wanne waliobaki walihukumiwa miezi mitatu jela na faini ya dola 130, kwa mujibu wa wakili Naima El Guellaf aliyeliambia shirika la habari la Associated Press.
Mmoja wa washtakiwa alizimia baada ya kusikia hukumu. Wengine walikataa kusimama kutoka kwenye benchi la washtakiwa walipoelekezwa kuelekea kwenye chumba kidogo cha mahabusu. Aidha ndugu zao, wakiwa na mshtuko mkubwa, walisisitiza kuwa jamaa zao hawana hatia.
Mawakili wa utetezi walisema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wanaouona kuwa mkali kupita kiasi.
Washtakiwa hao walikamatwa mwezi uliopita baada ya mashabiki wenye hasira kujaribu kuvamia uwanja wakipinga penali ya dakika za mwisho iliyotolewa kwa wenyeji Morocco katika fainali hiyo, ambayo Senegal iliibuka mshindi kwa bao moja sufuri. Mashabiki hao walizuiliwa rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja wakisubiri hukumu.
Katika kikao cha siku Alhamisi, kilichohudhuriwa na wanadiplomasia wa Senegal na Ufaransa pamoja na ndugu wa baadhi ya washtakiwa, mawakili walidai kuwa mahakama haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani mashabiki hao.
Mwendesha mashtaka wa serikali aliomba adhabu ya juu zaidi dhidi ya mashabiki hao, akisema walivuruga utaratibu wa mechi hiyo. Aliongeza kuwa uharibifu uliotokea unakadiriwa kufikia zaidi ya dola 476,719.
Morocco imekuwa ikikabiliwa kwa muda mrefu na matukio ya uhuni yanayohusiana na soka, na mara kwa mara mahakama zake hushughulikia kesi za aina hiyo. Hata hivyo, kesi hii ilikuwa ya kipekee kwa kuwa ilihusisha raia wa kigeni pekee.
Mwezi uliopita, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitoza faini ya dola milioni 1 na kutoa adhabu dhidi ya Senegal na Morocco kutokana na vurugu za mechi hiyo. Morocco imetangaza kuwa inapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, ikidai kuwa adhabu hizo hazilingani na matukio yaliyotokea.