Makamu wa Rais wa Uturuki akutana na balozi wa Brazil
Kikao chao kiliangazia ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili na uratibu wa Mkutano ujao wa COP31, ambapo Uturuki itakuwa mwenyeji.
Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz amempokea balozi wa Brazil nchini humo Gilda Motta Santos Neves, huku wawili hao wakijadiliana mahusiano kati ya nchi hizo pamoja na ushirikiano wao, kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi utakaofanyika mwezi Novemba 2026, nchini Uturuki.
Kupitia mtandao wa kijamii uitwao NSosyal, wa nchini Uturuki, siku ya Jumatatu, Yilmaz alieleza kuwa, kikao hicho kilichofanyika katika Ikulu ya Ankara, kiliangazia masuala mbalimbali, yakiwemo umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika miundombinu, sekta ya ulinzi, teknolojia, uwekezaji, pamoja na uratibu wa mkutano wa COP31.
Kulingana na Yilmaz, Brazil ni mdau muhimu, akiongeza kuwa Uturuki itaendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hizo, zitahusisha uanzishwaji wa mchakato wa uhusiano kati ya Uturuki na Brazil.
Yilmaz aliongeza kuwa, nchi hizo mbili zinafanya jitihada za kuongeza ujazo wa biashara, ili ufikie lengo la Dola Bilioni 10.
Kwa namna ya kipekee, Yilmaz alimshukuru balozi huyo kwa kumtembelea.