| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Uturuki na Qatar zasaini makubaliano ya ulinzi jijini Istanbul
Uturuki na Qatar pia zimesaini makubaliano mengine manne katika masuala ya biashara, elimu na diplomasia, kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Uturuki na Amir wa Qatar.
Uturuki na Qatar zasaini makubaliano ya ulinzi jijini Istanbul
Uturuki na Qatar zasaini mikataba 5 kufuatia mazungumzo kati ya Erdogan na Al Thani mjini Istanbul. / / AA

Uturuki na Qatar zimesaini makubaliano ya ulinzi, pamoja na mikataba mingine minne, baada ya mkutano wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, jijini Istanbul.

Katika taarifa iliyochapishwa kupitia mtandao wa kijamii wa X siku ya Ijumaa, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema kuwa Rais Erdogan alieleza kwamba makubaliano ya ulinzi yaliyosainiwa siku hiyo yataimarisha mwelekeo mpya katika uhusiano wa kindugu kati ya mataifa hayo mawili.

“Rais Erdogan amesisitiza umuhimu wa Uturuki na Qatar kuendelea kushirikiana katika kuzuia kurejea kwa vita katika eneo la Ghuba, kuongeza juhudi za mazungumzo na kufanikisha amani”, taarifa hiyo iliongeza.

Aidha, Erdogan alisisitiza umuhimu wa kuyashawishi mataifa yanayohusika kutatua tofauti zao kupitia njia za kidiplomasia.

Katika mazungumzo yake na Amir wa Qatar yaliyofanyika katika Ikulu ya Dolmabahce jijini Istanbul, Erdogan alijadili uhusiano wa mataifa hayo mawili pamoja na masuala mbalimbali yanayojiri katika kanda na dunia.

Erdogan amesema Mkataba wa Ushirikiano wa Biashara na Uchumi, ulioanza kutekelezwa mwaka uliopita, umeziwezesha nchi hizo kukaribia lengo lao la kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Pia alisema kuwa Uturuki inaendelea na juhudi za kuimarisha na kupanua ushirikiano wake na Qatar katika sekta ya nishati, huku akiongeza kuwa ushirikiano katika sekta ya viwanda vya ulinzi utaendelea kukua.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa

Mbali na makubaliano ya ulinzi, Uturuki na Qatar zilisaini makubaliano mengine manne katika sekta ya biashara, elimu na diplomasia, kufuatia mazungumzo kati ya Rais Erdogan na Amir wa Qatar.

Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Ikulu ya Rais ya Dolmabahce jijini Istanbul, baada ya mazungumzo ya faragha na yale yaliyohusisha wajumbe wa pande zote mbili, katika mkutano wa 12 wa Kamati ya Pamoja ya Kimkakati ya Ngazi ya Juu kati ya Uturuki na Qatar.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, na Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, walitia saini hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano katika masuala ya amani, maridhiano na utatuzi wa migogoro.

Mawaziri hao wawili pia walitia saini tamko la pamoja kufuatia mkutano wa 12 wa kamati hiyo.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Biashara wa Uturuki, Omer Bolat, na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Qatar, Sheikh Faisal bin Thani bin Faisal Al Thani, walitia saini hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano katika masuala ya ulinzi wa haki wa wanunuzi, ufuatiliaji wa shughuli za soko na ukaguzi.

Aidha, Waziri wa Elimu wa Uturuki, Yusuf Tekin, na Waziri wa Nchi wa Qatar, Mohammed bin Abdulaziz Al-Khulaifi, walitia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya elimu.

Kabla ya mazungumzo hayo, Rais Erdogan alimkaribisha Amir wa Qatar kwa hafla rasmi katika Ofisi ya Rais ya Dolmabahce jijini Istanbul.

Katika mazungumzo hayo, waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, pamoja na Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Uturuki (MIT), Ibrahim Kalin.

CHANZO:AA