Mifumo ya usalama ya Ulaya 'haitofanikiwa' bila Uturuki: Erdogan

Rais wa Uturuki ametoa wito wa ushirikiano zaidi katika masuala ya ulinzi Ulaya, aangazia ushirikiano unaimarika wa Uturuki na Afrika, na kutaka kuwepo kwa majadiliano katika mizozo ya kikanda kutoka Syria hadi Iran na Gaza.

By
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akizungumza na waandishi ndani ya ndege akitoka Ethiopia. (Picha: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki) / Wengine

Bara Ulaya haliwezi kuwa na mfumo sahihi wa usalama bila mchango wa Uturuki, Rais Recep Tayyip Erdogan ameonya, akieleza kuwa imefika wakati wa bara hilo kujumuisha Uturuki kikamilifu katika mifumo yake ya ulinzi na usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege katika safari yake kutoka Ethiopia siku ya Jumatano, Erdogan alisema Ulaya iachane na kile alichokieleza kuwa vikwazo vya kiitikadi vinavyozuia ushirikiano wa karibu na Uturuki. 

Alisisitiza kuwa jeshi la Uturuki ni miongoni mwa vikosi vyenye uwezo mkubwa NATO na kuonya kuwa mfumo wowote mpya wa Usalama Ulaya unaotenga Uturuki hautofanikiwa.

“Kama Ulaya ina nia ya kuwa na mfumo mpya thabiti wa ulinzi, ni wazi kuwa mipango bila kujumuisha Uturuki haitofanikiwa,” alisema, akiongeza kuwa uwezo wa Uturuki wa kijeshi uwanjani ni zaidi ya mshirika“ambaye anazungumza tu anapokuwa mezani.”

Kuimarisha ushirikiano na Afrika

Kuhusu ziara yake ya nchini Ethiopia, Erdogan alieleza nchi hiyo kama njia muhimu ya ushirikiano zaidi na bara la Afrika na kueleza nafasi ya Uturuki katika kujenga imani kwenye kanda, ikiwemo juhudi za upatanishi kati ya Ethiopia na Somalia. 

Alisema ziara hiyo imeonesha sera ya muda mrefu ya Uturuki ya ushirikiano na bara la Afrika kwa kuzingatia kuheshimiana na wala siyo kukandamiza.

“Uturuki haijawahi kuwa wakoloni wa Afrika,” alisema, akiongeza kuwa mtazamo wa nchi kwa ushirikiano wa usawa na diplomasia ya kusaidia watu umeimarisha nafasi yake katika bara.

Usalama nchini Syria na Iran

Kuhusu Syria, Erdogan amesema juhudi za Uturuki za kuwa na kanda “isiokuwa na ugaidi” zinaendelea kwa makini na yanayoendelea ndani ya Syria ni ishara ya kuanza kuonesha matokeo ya Uturuki kulipa suala la usalama kipaumbele. 

Alisema taasisi za Uturuki zinafuatilia kwa karibu juhudi za kujumuisha na kuendeleza mipango ya kisheria na kisiasa kwa lengo la kutambua chanzo cha mapigano, siyo tu masuala ya usalama.

Akizungumzia kuhusu mvutano kati ya Iran na Marekani, Erdogan anasema Uturuki inawasiliana na pande zote mbili na inapinga kufikia makabiliano ya kijeshi. 

Alisema hivi karibuni kwa nyakati tofauti alizungumza na uongozi wa Iran na Rais wa Marekani Donald Trump, akisisitiza kuwa majadiliano bado ndiyo njia pekee ya kuimarisha hali.

“Vita vingine vinavyolenga Iran havitomfaidi yeyote,” alisema, akionya kuwa hali hiyo itasababisha ukosefu zaidi wa usalama katika kanda. “ Madamu diplomasia inawezekana, bado kuna matumaini.”

Uturuki itahudhuria mkutano wa amani wa Gaza

Kuhusu Gaza, Erdogan alieleza mapigano hayo kama “majaribio kwa mazingatio ya utu,” akitoa wito wa kusitishwa kabisa mapigano, kuruhusu misaada kwa watu kuingizwa bila vizuizi na kuanzisha tena mchakato wa suluhu ya mataifa mawili. 

Alisema Uturuki itashiriki katika mkutano ujao wa amani na kuthibitisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan atahudhuria mkutano wa amani wa Gaza kwa niaba ya Uturuki.