Siku ya Jumanne Umoja wa Mataifa ulimuwekea vikwazo Algoney Hamdan Daglo Musa, mdogo wake mkuu wa wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan, na mamluki watatu wa Colombia wakishtumiwa kuwasajili wanajeshi wa zamani wa Colombia kupigana vita nchini Sudan.
Taarifa kutoka kwa ujumbe wa Uingereza kwa Umoja wa Mataifa umesema vikwazo hivyo vimewekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia mapendekezo ya Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Miongoni mwa waliowekewa vikwazo hivyo ni pamoja na Algoney Hamdan Daglo Musa, mdogo wake kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo. Unasema aliongoza harakati za kununua silaha na vifaa vya kijeshi kwa RSF.
Pia wengine waliowekewa vikwazo ni Alvaro Andres Quijano Becerra, Claudia Viviana Oliveros Forero, na Mateo Andres Duque Botero. Unasema walihusika katika kusajili wanajeshi wa zamani wa Colombia.
Ushahidi wa video na picha unaonesha raia watatu wa Colombia "wakiwapa mafunzo ya mbinu na kiufundi RSF, wakiwa pamoja na vikosi, marubani wa droni, kuendesha magari, na wakufunzi, na wengine pia wakiwafundisha watoto kupigana miongoni mwa vikosi vya RSF."
Mwezi Februari Uingereza, pamoja na Ufaransa na Marekani, walifanikiwa kuwawekea vikwazo makamanda wa RSF kwa ukatili uliofanywa na RSF katika kuzuia watu mji wa Al Fasher.
Mamluki wa Colombia wameshiriki katika vita kadhaa kote nchini Sudan, ikiwemo mji mkuu, Khartoum, Omdurman, Kordofan, na Al Fasher.
Vita hivyo vya miaka mitatu kati ya jeshi la Sudan na RSF vimesababisha kile mashirika ya misaada yanasema hali mbaya zaidi kwa watu duniani.
Mapema mwezi Aprili, Marekani iliweka vikwazo kwa makampuni matano na watu binafsi ambayo wanasema yalihusika katika kuwasajili wanajeshi wa zamani wa Colombia kupigana kwa niaba ya RSF. Inasema mamia ya wanajeshi wa zamani wa Colombia wameenda Sudan kusaidia RSF.


















