Mtu 1 auawa, wengine kadhaa wajeruhiwa katika shambulio la droni la RSF eneo la Kurmuk, Sudan

Gavana anasema ndege hizo zisizokuwa na rubani zililenga maeneo ya makazi ya watu; kundi hilo la wapiganaji halijatoa taarifa yoyote

By
Mashambulizi nchini Sudan. /Picha:Maktaba

Mtu mmoja ameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani yaliyofanywa na wapiganaji wa RSF katika mji wa Kurmuk jimbo la kusini mashariki la Blue Nile nchini Sudan, gavana wa mji huo alisema Alhamisi.

Abdelati Mohamed Al-Faki alisema katika taarifa kuwa ndege zisizokuwa na rubani za RSF zilishambulia mitaa ya makazi ya watu huko Kurmuk Jumatano jioni, akieleza mashambulio hayo kuwa yalilenga raia na mali zao kwa makusudi.

Anasema mashambulizi hayo yalisababisha kifo cha raia mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa, bila kueleza idadi kamili ya wale waliojeruhiwa. Mashambulizi hayo pia yalitatiza shughuli katika mtambo mmoja wa kusaga, aliongeza.

Al-Faki ameshtumu kile alichokieleza kuwa mashambulizi ya RSF na washirika wake, Sudan People’s Liberation Movement-North.

Hata hivyo, alisema kwa sasa hali eneo la Kurmuk imedhibitiwa na Jeshi la Sudan linahakikisha kuwa kuna usalama sehemu hiyo.

Hakukuwa na taarifa kutoka kwa RSF kuhusu matamshi ya gavana.