Wanajeshi wa Marekani kutoa mafunzo ya kupambana na ugaidi kwa vikosi vya Nigeria
Jeshi la Marekani linasema litawapa Nigeria taarifa za kijasusi kwa ajili ya mashambulizi ya angani na kuwasaidia katika ununuzi wa silaha.
Marekani itapeleka wanajeshi 200 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa vikosi vya Nigeria katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi, maafisa wa Nigeria na Marekani wamesema siku ya Jumanne, huku Marekani ikiimarisha ushirikiano wa kijeshi na taifa hilo la Afrika Magharibi.
‘‘Wanajeshi wa Marekani watatusaidia katika mafunzo na masuala ya kiufundi’’, Meja Jenerali Samaila Uba, msemaji wa Makao Makuu ya Jeshi la Nigeria, ameiambia AFP.
Shinikizo la kidiplomasia
Msemaji wa Kamandi ya majeshi ya Marekani kwa ajili ya Afrika amethibitisha kwa AFP kuhusu taarifa hizo.
Nigeria imekuwa ikishinikizwa kidiplomasia na Marekani kuhusu usalama ndani ya nchi hiyo, ambao Rais wa Marekani Donald Trump ameeleza kuwa ‘‘unyanyasaji’’ na ‘‘mauaji ya halaiki’’ dhidi ya Wakristo.
Pamoja na kuwepo kwa matukio ya Wakristo kushambuliwa, idadi kubwa ya Waislamu pia wanauawa, huku mshauri mwandamizi wa Trump kuhusu masuala ya Arabuni na Afrika, Massad Boulos, akisema mwaka uliopita, kuwa magaidi wa Boko Haram na Daesh ‘‘wanaua Waislamu wengi zaidi kuliko Wakristo.’’
Nigeria inakanusha madai ya kuwanyanyasa Wakristo nchini mwao, simulizi ambayo Marekani imekuwa ikiiendeleza kwa muda mrefu.
Nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya raia barani Afrika imekuwa ikikabiliana na magaidi kwa muda mrefu kaskazini mashariki mwa nchi, huku magenge mengine yasiyokuwa na itikadi yoyote kali yakiteka watu nyara kwa ajili ya kulipwa kikombozi na kupora mali za watu katika vijiji vya kaskazini magharibi.